Afisa wa polisi na mwanafunzi washtakiwa kwa wizi wa pombe
Na LAWRENCE ONGARO
AFISA mmoja wa polisi na mwanafunzi wa chuo kikuu wamefikishwa mahakamani kwa wizi wa pombe kutoka katika kiwanda cha Thika.
Afisa huyo Bi Anastacia Muchungu na mwanafunzi huyo, Ben Kamau, walifikishwa mbele ya hakimu mkuu wa Thika Bw Oscar Wanyaga, wakituhumiwa kwamba walipatikana na katoni 11 za pombe aina ya whisky chapa ‘Furaha’ kutoka kiwanda cha African Spirits Limited mjini Thika.
Inadaiwa kuwa kiwanda hicho kilifungwa Januari 2019 baada ya kukosa kulipia ushuru ya mamilioni ya fedha.
Kulingana na maelezo yaliyokuwa katika faili ya washtakiwa ni kwamba mnamo Januari 4, 2020, wawili hao waliingia katika kiwanda hicho cha mvinyo na kuiba katoni 11 za whisky chapa ‘Furaha’ wakitumia gari aina ya Toyota Premio nambari KBP 770D.
Gari hilo lilinaswa katika kizuizi cha Polisi cha Makongeni mjini Thika likisafirisha pombe hiyo.
Miezi michache iliyopita inadaiwa afisa mwingine wa polisi alifariki katika kiwanda hicho akishika doria baada ya kudaiwa alianguka kutoka ghorofa ya juu.
Afisa anayechunguza kesi hiyo aliomba mahakama iruhusu ombi lake la kutaka washukiwa wasalie kizuizini kwa siku zingine saba huku akifanya uchunguzi zaidi.
Lakini hakimu huyo alikubali ombi la washukiwa na kuwaachilia kwa dhamana ya Sh100,000 na mdhamini wa kiwango sawa ama dhamana ya Sh50,000 pesa taslimu kila mmoja.
Kulingana na uamuzi wake hakimu huyo, hata ingawa afisa huyo wa kuendesha uchunguzi alikuwa na nia waendelee kuzuiliwa kwa muda huo, bado ni vyema kuzingatia haki zao za kimsingi ambazo ziko kwenye Katiba.
Kwa hivyo alitoa amri washtakiwa washtakiwe haraka iwezekanavyo ili wawe nje kwa dhamana wakingoja kuendelea kwa kesi hiyo.
Afisa anayeendesha uchunguzi huo Bw Pascal Omondi alisema bado kuna washukiwa wengine anaotarajia kufikisha mahakamani ili kujumuishwa na washukiwa hao wawili.
Alitaka apewe muda wa siku saba ili aweze kukamilisha uchunguzi wake na kuwafikisha mahakamani.
Hata hivyo, hakimu alipanga kesi hiyo kutajwa Januari 14, 2020, huku washukiwa wakiwakilishwa na wakili wao Bw Ishmael Nguring’a.
Washukiwa hao walifika mahakamani wakijifunika nyuso zao ili wasichukuliwe picha na waandishi wa habari.
Mahakama ilijaa pomoni huku watu waliofika huko wakitaka kujionea washukiwa hao ambao walikuwa chini ya ulinzi mkali.