• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 7:55 AM
Mshukiwa wa Al-Shabaab ajisalimisha kanisani

Mshukiwa wa Al-Shabaab ajisalimisha kanisani

Na BRIAN OCHARO

MWANAMUME ambaye anashukiwa ni mwanachama wa zamani wa kundi la kigaidi la al-Shabaab, alijitokeza kanisani kutubu na kuombewa kabla ya kujisalimisha kwa polisi.

Mshukiwa huyo ambaye alifika katika kanisa Kaunti ya Kilifi mnamo Januari 3, anaripotiwa kutubu na kuomba kusaidiwa kupata wokovu.

Kulingana na wachunguzi, mshukiwa huyo ambaye ana umri wa miaka 30, alimuomba askofu wa kanisa hilo kumsaidia kurudi kufanya mapenzi ya Mungu.

Baada ya kufanya maombi, askofu wa kanisa hilo alimsindikiza hadi katika kituo cha polisi ambako aliandikisha taarifa kisha akakamatwa.

Polisi wanasema uchunguzi wa umeonyesha alikuwa ametorokea Somalia ambako alipata mafunzo kutoka kwa wanamgambo wa al-Shabaab kabla ya kurejea Kenya

“Baada ya kurejea nchini, mshukiwa alibadili nia na kuamua kutafuta msaada kanisani. Alitubu dhambi zake na kuomba kufanyiwa maombi ili aweze kuokoka,” mdokezi alisema.

Mshukiwa huyo ambaye kwa sasa anawasaidia polisi katika uchunguzi alifikishwa katika mahakama ya Mombasa mnamo Jumanne, ambapo wapelelezi waliruhusiwa kuendelea kumzuia kwa siku 10 huku uchunguzi ukiendelea.

Afisa wa upelelezi, Bw David Mureithi aliiambia mahakama kuwa wanahitaji muda zaidi kukamilisha uchunguzi wao kwani mshukiwa huyo anaaminika kuwa na taarifa muhimu ambayo inaweza kuwasaidia kuwakamata washukiwa zaidi.

Bw Masila alisema kuwa huenda mshukiwa huyo akashtakiwa na kosa la kuwa mwanachama wa al-Shabaab.

Mshukiwa huyo alijisalimisha kwa polisi siku mbilli baada ya mshukiwa mwingine wa kundi hilo, Omar Salim Unda kuuawa katika eneo la Dabaso, Kaunti ya Kilifi.

Unda anadaiwa kuwa mwanachama wa zamani wa kundi hilo.

Kesi hiyo itatajwa tena Januari 23.

You can share this post!

Amsamehe aliyemdunga kisu

Wanafunzi wote kunufaika na bima ya afya

adminleo