• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 7:50 AM
Sina hela za kulisha familia, Sonko sasa alia

Sina hela za kulisha familia, Sonko sasa alia

MAUREEN KAKAH na SAM KIPLAGAT

GAVANA wa Nairobi, Mike Sonko amelilia mahakama imhurumie kwa kuwa familia yake inateseka kwa kukosa pesa za matumizi.

Bw Sonko amewasilisha kilio kortini baada ya akaunti zake zote za benki kufungwa kuhusiana na kesi ya ufisadi dhidi yake, na hivyo hana uwezo wa kugharamia mahitaji ya kimsingi ya familia yake.

Desemba mwaka uliopita, mahakama iliagiza azuiwe kutumia akaunti hizo punde baada ya ya kushtakiwa kwa ufisadi.

Bw Sonko, ambaye ni maarufu kwa maisha ya kifahari, sasa ametaja hatua hiyo kuwa ya ukandamizaji na isiyo ya haki.

“Hana uwezo wa kugharamia mahitaji yake wala ya familia yake kwani hawezi kupokea hata mshahara wake kutoka kwa akaunti zake,” wakili Harrison Kinyanjui aliambia mahakama jijini Nairobi.

Hakimu Mkuu Mkaazi, Bi Elekta Riany alitoa agizo la muda mnamo Desemba 11, 2019, kumzuia Bw Sonko kutumia akaunti zake 15 zilizo katika benki tisa tofauti.

Agizo hilo pia liliruhusu Shirika la Kutwaa Mali za Umma zilizopatikana kwa Ufisadi (ARA), kuchunguza fedha zilivyoingizwa na kutolewa katika akaunti hizo tangu Januari 2017.

Shirika hilo lilipewa siku 90 kukamilisha shughuli hiyo.

Hakimu Mkuu Martha Mutuku aliagiza benki zote zalizotajwa zikabidhiwe nakala za kesi ili ziweze kujibu malalamishi ya Bw Sonko.

Hakimu Mutuku pia aliagiza wahusika wote katika kesi hiyo warudi mahakamani Januari 27 kujadili ombi hilo.

Benki hizo zinajumuisha KCB, Diamond Trust, I&M, Sidian, National Bank, Bank of Africa, Equity, Co-operative na Credit Bank.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) aliwasilisha mashtaka 19 dhidi ya Bw Sonko na washtakiwa wengine, akidai walihusika katika ufisadi na uporaji wa mali ya umma. Wote walikanusha mashtaka hayo kuhusu ufujaji wa Sh357 milioni.

Wakati ARA ilipoenda kortini Desemba ilisema huenda Bw Sonko na washtakiwa wengine wakatoa pesa katika akaunti zao na hivyo basi kutatiza upelelezi.

Mahakama pia iliombwa kuzuia utoaji pesa katika akaunti hizo kwa siku 90.

Kulingana na Bw Sonko, ARA haikutoa sababu zozote za kuridhisha wala ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa akaunti zake zilitumiwa kwa njia zilizokiuka sheria.

Aliongeza kuwa ARA haikuonyesha uhusiano kati ya pesa zilizo katika akaunti zake na zile zinazodaiwa kupotea kutoka kwa serikali ya kaunti.

You can share this post!

Mzozo wa Iran na Amerika hautaathiri Kenya, ubalozi wa Iran...

Wazee walaani serikali kumtesa Miguna

adminleo