• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 2:18 PM
Malumbano yachacha vikao vya BBI vikianza

Malumbano yachacha vikao vya BBI vikianza

CHARLES WASONGA, RUTH MBULA na BRIAN OJAMAA

MALUMBANO kuhusu msururu wa mikutano ya kutoa hamasisho kuhusu mapendekezo ya ripoti ya jopo la maridhiano (BBI) yaliendelea kuchacha jana muda mchache kabla ya mkutano wa kwanza kuanza leo mjini Kisii.

Alhamisi, kundi la viongozi kutoka magharibi mwa Kenya walishilikia kuwa mkutano uliopangiwa kufanyika mjini Kakamega mnamo Januari 18 utaendelea kama ulivyopangwa licha ya pingamizi zilizoibuliwa na wenzao mnamo Jumatano.

Wakiongozwa na Seneta wa Kakamega Cleophas Malala, wanasiasa hao walisema mkutano wa maandalizi utafanyika Jumapili Bungoma ambapo jumla ya viongozi 500 watashiriki.

Alisema viongozi wakaohudhuria mkutano huo, katika ukumbi wa kampuni ya Sukari ya Nzoia, wataandaa memoranda yenye masuala muhimu yatakayowasilishwa katika mkutano wa BBI Kakamega.

“Wale wanaopinga mkutano wa BBI utakaofanyika uwanjani Bukhungu mjini Kakamega wanaendeleza maslahi ya mkubwa wao asiyetaka mabadiliko. Alifeli mnamo 2010 alipopinga mageuzi na tunamhakikishia kuwa atafeli tena,” Bw Malala akasema kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi.

Aliandamana na wabunge, Godfrey Osotsi (mbunge maalum, ANC), Chris Omulele (Luanda), Elsie Muhanda (Mbunge Mwakilishi, Kakamega), Florence Mutua (Mbunge Mwakilishi, Busia), Ayub Savula (Lugari) miongoni mwa wengine.

Seneta Malala ambaye ni naibu kiongozi wa wachache bungeni, alikariri kuwa viongozi wa matabaka yote na wananchi wa kawaida wamealikwa katika mkutano. Lakini Jumatano, wabunge 12 kutoka eneo la Magharibi walipendekeza mkutano huo uahirishwe wakidai kutoshirikishwa katika maandalizi yao.

Wakiongozwa na Mbunge wa Nambale Sakwa Bunyasi wabunge kutoka vyama vya Jubilee, ANC na Ford Kenya, waliongeza kuwa siku hiyo wamepanga kukutana na mrasimu wa kampuni ya Sukari ya Mumias kujadili hatua ambazo zimepigwa kuifufua.

“Tunahisi kuwa waandalizi wa mkutano wa Kakamega wanalenga kuendeleza ajenda fiche ya chama cha ODM wala sio kujadili ripoti ya BBI inavyodaiwa. Hatuwezi kuhudhuria mkutano ambao ni dhahiri kwamba unalenga kuendeleza masilahi ya kisiasa ya watu kutoka nje,” akasema Bunyasi.

Vile vile, baadhi ya madiwani kutoka kaunti ya Bungoma pia wameapa kutohudhuria mkutano huo wa Kakamega wakidai umepanga na Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli kwa lengo la kuhujumu viongozi wa eneo hilo.

Wakiongozwa na diwani Francis Chemion wa wadi ya Kaptama kutoka eneo bunge la Mlima Elgon, walidai mkutano huo unalenga kumfanyia kampeni kiongozi wa ODM Raila Odinga katika eneo la Magharibi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Na mkutano wa leo mjini Kisii, utakaohudhuriwa na magavana sita kutoka Nyanza umepingwa na baadhi ya wanasiasa wa eneo hilo wakiongozwa na Naibu Gavana Joash Maangi aliyedai ni “kupoteza pesa bila sababu.”

Hata hivyo, Gavana James Ongwae ambaye ndiye mwenyeji wa mkutano huo ameshikilia kuwa utaendelea ulivyopangwa licha ya pingamizi hizo.

“Mkutano huu unalenga kutoa uhamisisho kuhusu mapendekezo yaliyoko kwenye ripoti ya BBI. Kuna mengi katika ripoti hiyo yenye manufaa kwa zaidi kwa watu 9 milioni katika eneo la Nyanza na ambayo yataainishwa katika mkutano huo,” akasema Bw Ongwae.

Mkutano huo utahudhuriwa na magavana; Peter Anyang Nyong’o (Kisumu), John Nyarama (Nyamira), Cornel Rasanga (Siaya), Okoth Obado (Migori) na Cyprian Awiti (Homa Bay). Duru zilisema kuwa Bw Odinga pia anatarajiwa kuhudhuria.

You can share this post!

Msomi Prof Euphrase Kezilahabi aombolezwa

Masharti kwa wanachama wapya wa NHIF

adminleo