Dondoo

Lofa apasua kuni kama adhabu ya kula vya bwerere

April 11th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na TOBBIE WEKESA

GIKOMBA, NAIROBI

Kalameni mmoja aliwaacha watu vinywa wazi mkahawani alipodai kwamba hakuwa na hela za kulipia chakula alichotumbukiza tumboni.

Inasemekana kalameni aliingia katika mkahawa huo huku akionyesha sura ya mtu mwenye hela na kuitisha ugali kwa samaki.

Baada ya kumaliza kula,  aliinuka polepole huku akijinyoosha na kuelekea hadi kwenye kaunta.

“Keshia alimuitisha risiti. Polo aliitoa na kumpokeza,” alieleza mdokezi. Weita aliyemhudumia alikuwa nyuma yake kuthibitisha kwamba alitoa hela alizohitajika kulipia.

“Umekula chakula cha Sh250. Hebu lipa,” weita alimueleza polo. Jamaa alimuangalia weita kwa jicho la huruma.

“Mimi sina pesa zozote. Niko tayari kuwapasulia kuni hata mpaka kesho mkitaka,” jamaa alidai. Keshia alimkemea huku akimvuta nyuma ya hoteli.

“Mimi nimewaambia sina pesa. Mlitaka nife kwa sababu ya njaa na chakula kimejaa hapa,” polo alisema kwa sauti ya juu. Wateja waliokuwa mkahawani walibaki wakiangua vicheko.

“Hakuna kuni utakazopasua hapa. Wewe lazima ulipie chakula ulichokula,” keshia alimueleza jamaa kwa ukali.

Wateja waliokuwa mkahawani walishangaa kwa nini jamaa hakusema mapema hakuwa na pesa mfukoni ili asaidiwe. Duru zinasema mwenye hoteli alipoingia, polo alipewa shoka na upanga na kuagizwa aanze kupasua kuni.

“Wewe hatutakuruhusu uende. Utakaa hapa hadi umalize juma moja ukipasua kuni. Isitoshe, nisikupate umekaribia jikoni. Wewe unaweza kula chakula chote,” polo alionywa na mwenye hoteli.

Baada ya saa tano kwenye kibarua, polo aliomba msamaha huku akiahidi kutorudia tendo hilo. Hata hivyo, hakuna aliyemhurumia akiambiwa hayo yalikuwa masaibu ya kujitakia mwenyewe. Alipasua kuni hadi mkahawa ulipofungwa.

…WAZO BONZO…