Jaji asimamishwa kazi kwa madai ya kushiriki ngono kortini
MASHIRIKA na CHARLES WASONGA
JAJI mmoja, wa kike, wa Mahakama ya kusikiza kesi za kifamilia jijini Kentucky amesimamishwa kazi kwa tuhuma za kujihusisha na mienendo mibaya, ikiwemo kushiriki ngono na wanaume wawili kwa mpigo ndani ya korti.
Bi Dawn Gentry, jaji wa mahakama hiyo inayopatikana katika eneo la Kenton, kaskazini mwa Kentucky alishtakiwa kwa makosa mbalimbali ya utovu wa nidhamu mnamo Novemba mwaka jana na Kamati ya Kufuatilia Mienendo ya Maafisa wa Mahakama.
Alisimamishwa kazi wiki hii kusubiri uamuzi wa mwisho wa kamati hiyo kuhusu suala hilo.
Gentry analaumiwa kwa kuwashinikiza wafanyakazi wa mahakama kuhudumu katika kamati iliyosimamia kampeni za kupigia debe kuchaguliwa kwake kama jaji.
Pia anadaiwa kumkodi mwanamume mmoja ambaye alishiriki ngono naye, kwa mujibu wa stakabadhi za kamati hiyo. Alikana madai yote dhidi yake.
Jaji huyo ambaye alichaguliwa mnamo Novemba 2018 anadaiwa kumwajiri mpenzi wake, pasta wa zamani, na akamruhusi kucheza gitaa na kuimba afisini mwaka na hivyo kuwasababisha usumbufu kwa wafanyakazi wa mahakama, kulingana na stakabadhi hizo.
Lakini wakili wa Gentry alimtetea akisema kuwa jaji huyo hakufahamu kwamba mwenendo wa mwanamume huyo ulisababisha usumbufu, stakabadhi hizo zinaonyesha.
Aidha zinasema kuwa Gentry, mpenzi wake wa kiume na mfanyakazi mwingi wa mahakama, ambaye ni mwanamke, wanadaiwa kushiriki ngono ndani ya korti, madai ambayo jaji huyo amekana vikali.
Vile vile, anakabiliwa na makosa ya kuwaruhusu watoto wake kuhudhuria vikao faragha vya mahakama vilivyowahusisha watoto wengine pamoja na kuwaruhusu baadhi ya wafanyakazi wa mahakama kubugia pombe mahakamani.
Lakini wakili wa Gentry, Stephen Ryan alisema, kwenye mahojiano Jumatano, kwamba waliohudhuria vikao vya mahakama walifurajiwa na weledi wa Gentry kama jaji na hivyo hafai kusimamishwa kazi.