• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
Tangatanga wachemka Kuria akilala ndani wikendi

Tangatanga wachemka Kuria akilala ndani wikendi

Na BENSON MATHEKA

KUNDI la wabunge wanaomuunga Naibu Rais William Ruto, maarufu kama Tangatanga,  limelaumu serikali kwa kuwahangaisha kufuatia kukamatwa kwa mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria kwa madai ya kushambulia mwanamke jijini Nairobi.

Wabunge waliomtembelea Bw Kuria katika seli za kituo cha polisi cha Kilimani, Nairobi walisema kukamatwa kwa mbunge ni njama ya kumtisha akome kumuunga Dkt Ruto.

Bw Kuria, aliyekamatwa Ijumaa asubuhi atalala seli za polisi wikendi hii hadi Jumatatu anapotarajiwa kufikishwa kortini kujibu mashtaka ya kumshambulia mwanamke katika studio za shirika la habari la Royal Media Services jijini Nairobi Desemba 2019.

Alikamatwa kufuatia malalamishi ya Bi Joyce Wanja almaarufu Wagichungumwa kwamba alimshambulia makusudi walipokutana katika studio hizo.

Wanja ambaye ni mwanaharakati kaunti ya Kiambu, alikuwa amefahamisha kituo kimoja cha runinga kwamba alikuwa amealikwa katika studio za runinga ya Inooro TV kushiriki kipindi cha siasa mbunge huyo alipomchapa.

Alisema Kuria alikasirika alipomtaka kuomba msamaha kwa kutoa matamshi ya kudhalilisha wanawake kwenye hafla moja kaunti ya Kiambu iliyohudhuriwa na watoto.

“Matamshi yake yalikuwa ya kudhalilisha wanawake tena mbele ya watoto na ndio maana nilimweleza kwamba anafaa kufikiria kuyaondoa matamshi hayo lakini badala ya kufanya hivyo alinishambulia,” alisema kwenye kanda ambayo imesambazwa kwa wingi katika mitandao ya kijamii.

Jana, mkuu wa polisi eneo la Nairobi, Philip Ndolo alisema kwamba Kuria atapelekwa kortini Jumatatu. Wabunge kadhaa wa Tanga Tanga wakiongozwa na mbunge wa Kikuyu Kamau Ichungwa na mwenzake wa Kiharu Ndindi Nyoro waliomtembelea kituoni walipuuza madai ya mwanamke huyo na kusema kukamatwa kwa Kuria kunahusiana na msimamo wake wa kisiasa.

Bw Ichungwa alidai kwamba masaibu ya Kuria yanatokana na kauli zake za kukosoa maamuzi ya serikali hasa kuhusu Jopokazi la Maridhiano (BBI). Alisema lengo ni kuwatisha wanaomuunga Ruto ili wajitenge naye.

Hii sio mara ya kwanza Bw Kuria kulala seli za polisi akiwa mbunge. Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017 alikamatwa pamoja na wabunge wengine na kushtakiwa kwa kutoa matamshi ya uchochezi.

You can share this post!

BBI ni daraja la Canaan – Raila

Serikali yataka Sonko atupwe ndani pia

adminleo