• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Kuria aagizwa kufika mbele ya kamati ya IEBC

Kuria aagizwa kufika mbele ya kamati ya IEBC

NA CHARLES WASONGA

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imemwamuru Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria kufika mbele yake ili afafanue madai yake kwamba kura ziliibiwa katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Bw Kuria ambaye ni mwanasiasa anayezoea kutoa kauli za kuzua utata alitoa madai hayo katika uwanja wa Kasarani, wakati wa kongamano la wajumbe wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), Machi 15, 2022.

Katika barua aliyoandikiwa na kamati ya IEBC kuhusu udumishaji wa madili katika shughuli za uchaguzi, mbunge huyo anatakiwa kufika mbele yake mnamo Machi 30, 2022.

“Unahitajika kufika katika makao makuu ya IEBC katika jumba la Anniversary orofa ya sita mnamo Machi 30, 2022 saa nne za asubuhi kuchunguzwa na Kamati ya kuhakikisha uzingatiaji wa Maadili katika uchaguzi. Hii ni kuhusiana na madai uliyotoa wakati wa kongamano la wajumbe wa chama cha UDA katika uwanja wa Kasarani mnamo Machi 15, 2022,” IEBC ikaeleza katika barua yake kwa Bw Kuria.

Barua hiyo ilitiwa saini na Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Marjan Hussein Marjan ambaye juzi aliapishwa kuchukua rasmi wadhifa huo aliushikilia kama kaimu kwa miaka minne.

Kawaida, ni kwamba mwenyekiti wa kamati hiyo ya udumishaji maadili kuhusiana na masuala ya uchaguzi huwa ni mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati.

Mwanasiasa mwingine ambaye amefiki mbele ya kamati hiyo kuhusiana na madai hayo ya wizi wa kura ni Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Murang’a Bi Sabina Chege.

Mnamo Alhamisi Bw Chebukati aliambia Kamati ya Seneti kuhusu Haki na Masuala ya Sheria na Haki za Kibinadamu kwamba tume hiyo haiwezi kumwagiza Naibu Rais William Ruto kuhusiana na madai kama haya aliyotoa akiwa nchini Amerika.

Kulingana na mwenyekiti huyo, IEBC haina mamlaka ya kuchunguza madai yaliyotolewa nje ya nchi ya Kenya.

“Kwa sababu Dkt Ruto alitoa madai yake akiwa nje ya nchi, sisi kama tume hatuna uwezo wa kuyachunguza. Huo ni wajibu wa asasi nyingine za serikali kwa ushirikiano na Wizara ya Masuala ya Kigeni,” Bw Chebukati akaiambia kamati hiyo katika majengo ya bunge, Nairobi.

You can share this post!

Biden kuzuru mpaka wa Ukraine na Poland

Argentina wacharaza Venezuela katika mechi ya kufuzu kwa...

T L