• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:10 PM
Serikali yataka Sonko atupwe ndani pia

Serikali yataka Sonko atupwe ndani pia

 Na MAUREEN KAKAH

HUENDA kesi ya ufisadi inayomkabili gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko ikasikilizwa akiwa seli baada ya serikali kupitia Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Noordin Haji, kuomba mahakama ifutilie mbali dhamana yake.

Kulingana na stakabadhi zilizowasilishwa kortini na serikali, Bw Sonko alikaidi masharti ya dhamana yake kwa kuteua Naibu Gavana ilhali hafai kukanyaga ofisi yake alivyoagizwa na mahakama.

Kulingana na serikali, hatua ya Bw Sonko inahusiana na ofisi yake na ni sawa na kuvuruga ushahidi na anafaa kukamatwa na kutupwa rumande.

“Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma inathibitisha kuwa ombi hilo ni la dharura kustahili kusikilizwa na hakimu aliamua mara moja kwa sababu linahusu maslahi ya umma kwa sababu gavana amekiuka maagizo ya dhamana yake,” alisema wakili Joseph Riungu.

Aliongeza: “ Mahakama hii ifute dhamana aliyopewa gavana kwa sababu alienda kinyume na sheria na kukiuka masharti ya dhamana aliyokabidhiwa Desemba 11, 2019 alipoingia katika ofisi yake na kuteua naibu gavana wa kaunti ya Nairobi.”

Upande wa mashtaka pia unataka maafisa wa serikali ya kaunti ya Nairobi waagizwe kutomruhusu Bw Sonko kuingia katika ofisi yake.

Kulingana na Bw Riungu, kuna hatari ya wazi kwamba Sonko ataingilia, kutisha na kushawishi mashahidi ambao wako chini yake na kuvuruga kesi.

Katika ombi lake, Bw Haji anadai kuna ukiukaji wa wazi wa masharti ya dhamana na mahakama unafaa kuchukua hatua kesi ikiendelea.

Bw Sonko kupitia kwa wakili wake Cecil Miller anadai kwamba alikuwa akitekeleza majukumu yake alipomteua Anne Kananu Mwenda kuwa Naibu Gavana.

Kwenye barua kwa Bw Haji, Bw Miller anasema kuteua naibu gavana hakuhusiani na kesi inayomkabili Bw Sonko na kwamba kushtakiwa hakumaanishi aliondolewa mamlakani.

Kulingana na wakili huyo, mahakama ilimzuia Bw Sonko kukanyaga ofisi peke na sio kutekeleza majukumu yake. Sonko alishtakiwa mwaka jana na amekanusha mashtaka 19 ya ufisadi.

Upande wa mashtaka unadai aliwahi kutoroka gerezani kabla ya kukamilisha hukumu.

You can share this post!

Tangatanga wachemka Kuria akilala ndani wikendi

Majonzi kansa kunyakua mtangazaji maarufu

adminleo