• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Ruto aonya serikali dhidi ya kupuuza maagizo ya korti

Ruto aonya serikali dhidi ya kupuuza maagizo ya korti

Na GEORGE SAYAGIE

NAIBU Rais William Ruto amewaonya vikali maafisa wa serikali wanaopuuza maagizo ya mahakama huku akisema kuwa wataadhibiwa.

Akionekana kumshambulia Waziri wa Usalama, Fred Matiang’i na Katibu wa Wizara Karanja Kibicho, Dkt Ruto alisema maafisa hao wanachafua sifa ya serikali.

Dkt Ruto, aliyekuwa akizungumza katika Kanisa la African Gospel Church Bethel la Olerai katika Narok Magharibi, alionya kuwa maafisa hao wanatishia demokrasia kwa kupuuza Katiba na sheria.

Dkt Ruto alitoa onyo hilo siku mbili baada ya polisi kumkamata mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria Ijumaa na kukataa kumwachilia licha ya korti kuagiza aachiliwe kwa dhamana.

Bw Kuria alikamatwa kutokana na madai kwamba alishambulia mwanamke katika afisi za Royal Media Services, Desemba mwaka jana.

Mahakama iliagiza kuwa Bw Kuria aachiliwe kwa dhamana ya Sh50,000.

Hakimu Mkuu Kennedy Cheruiyot pia aliagiza kuwa mbunge huyo afikishwe kortini leo asubuhi.

Naibu wa Rais pia alisema hayo wiki moja baada ya serikali kukataa kumruhusu wakili Miguna Miguna, ambaye alifurushwa kwa nguvu na serikali hadi Canada mnamo 2018, kurejea tena humu nchini.

Hii ni licha ya kuwepo kwa maagizo kadhaa ya mahakama kwa serikali kumruhusu Bw Miguna kurudi nchini.

“Nawaonya kwamba afisa wa serikali anayekiuka sheria na kupuuza maagizo ya mahakama atabeba msalaba wake mwenyewe,” akasema Dkt Ruto.

You can share this post!

Ndoa ya unafiki

Waliokuwa wakitegemea misaada ya Sonko waumia

adminleo