Habari MsetoSiasa

Waliokuwa wakitegemea misaada ya Sonko waumia

January 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na COLLINS OMULO

UGUMU wa maisha ambao huandamana na mwezi wa Januari unaosababishwa na uhaba wa fedha umekumba mamia ya watu waliotegemea Gavana wa Nairobi Mike Sonko ambaye amepigwa marufuku na korti kwenda afisini kwake.

Tangu Bw Sonko kuzuiliwa kuingia afisini hadi pale kesi ya ufisadi inayomkabili itakaposikizwa na kuamliwa, afisi yake ya kibinafsi iliyoko katika eneo la Upper Hill, Nairobi, imesalia ‘mahame’.

Mamia ya watu waliofika afisini hapo kutafuta msaada wa kifedha sasa wamesalia mayatima kwani siku hizi haifunguliwi mara kwa mara tofauti na hapo awali.

Kabla ya kuzimwa, afisi hiyo ilionekana yenye shughuli nyingi kwani kila siku foleni ndefu ya watu waliokuwa wakingojea kupewa fedha kwa zamu.

Iwapo picha za video zilizonaswa na zaidi na kamera 20 za CCTV zilizoko kwenye afisi hiyo zitaonyeshwa, itafichua wanasiasa watajika, marafiki, wanahabari wanaoandika habari kwa kutegemea matumbo, viongozi wa mashirika ya kijamii na hata vijana wa kukodishwa kuzua vurugu wakiwa wamepanga foleni kwenda kusaka fedha kwa Gavana Sonko.

Hali imekuwa mbaya zaidi kufuatia hatua ya serikali kufunga akaunti zote za benki za Bw Sonko, wiki iliyopita.

Wanasiasa waliokuwa wakinufaika na fedha hizo za bwerere ni wale walioenda katika afisi hiyo ya kibinafsi kumwelezea Bw Sonko mambo ya siri ambayo ‘maadui wake wa kisiasa’ walikuwa wakipanga.

Kulingana na duru, Bw Sonko sasa anawakwepa wanasiasa hao ambao wanajumuisha madiwani wa Nairobi na wabunge.

Kwa sasa Gavana Sonko anaruhusu tu mawakili na mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Simon Mbugua kukutana naye.

Bw Mbugua ndiye anamsaidia kutafuta fedha za kujikimu tangu akaunti zake za benki kufungwa, kwa mujibu wa wandani wake waliozungumza na Taifa Leo.

Baadhi ya madiwani sasa wanampigia simu kumtaka kutoa fedha ili ‘tuandae vikao na wanahabari tukanushe madai ya kukuharibia sifa’.

“Kila wakati kulikuwa na foleni ya watu kwenye mlango wa afisi yake ya kibinafsi. Siku ya Ijumaa ndiyo ilikuwa na foleni ndefu zaidi. Lakini alipozimwa na korti kufika afisini kwake, aliwaambia rafiki zake wasimsumbue kwani anashughulikia kesi inayomkabili,” akasema mmoja wa wandani wake.

“Gavana anaendelea na maisha yake kama kawaida lakini ameshauriwa na mawakili wake kukoma kuhutubia wanahabari,” akaongezea.

Diwani wa Jubilee alifichua kuwa Gavana Sonko alikuwa akitumia Sh3 milioni kuwapa fedha za bwerere wanasiasa na makundi yanayomuunga mkono kwa siku.

“Madiwani walikuwa wakipata hela za bwerere kila siku kutoka kwa Bw Sonko. Kila diwani alipewa fedha zisizopungua Sh10,000,” akaongezea.

Makundi mengine yaliyoathiriwa ni pamoja na makundi yaliyompigia debe katika maeneo mbalimbali jijini, kikosi cha Ng’arisha Jiji ambacho kimekuwa kikifanya usafi, wanablogu wanaomtetea mtandaoni, na kadhalika.

Kabla ya kitumbua kuingia mchanga, makundi mbalimbali, wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu, yalihutubia wanahabari angalau mara tatu kwa siku kumtetea Sonko.

Watetezi wa Gavana Sonko wamehutubia wanahabari mara moja tu ndani ya miezi minne iliyopita, tangu Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi (EACC) kuanza kumwandama kutokana na madai ya kuhusika na ufisadi.