• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Presha yamzidi Sultan kaunti ikikosa mawaziri

Presha yamzidi Sultan kaunti ikikosa mawaziri

NA DIANA MUTHEU

GAVANA wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho anazidi kunyoshewa kidole cha lawama kwa kubakia kimya baada ya kukosa kutangaza mawaziri wapya.

Gavana huyo aliye maarufu kama Sultan, ameonekana akizunguka nchini akiendesha kampeni za ripoti ya BBI, huku shughuli za kaunti yake zikiendeshwa na maafisa wakuu wa kaunti.

Mnamo Jumatano, Bw Joho alijumuika pamoja na viongozi wengine huko Kisii katika hafla ya kwanza ya ripoti ya BBI.

Kinara wa chama cha ODM, Raila Odinga, waziri wa maswala ya ndani Fred Matiang’i, magavana Anne Waiguru (Kirinyaga) Anyang Nyongo (Kisumu), Okoth Obado (Migori) na Sospeter Ojamong (Busia).

Magavana wengine waliohudhuria hafla hiyo ni John Nyagarama (Nyamira), Amason Kingi (Kilifi), Wycliffe Oparanya (Kakamega), James Ongwae(Kisii) miongoni mwa viongozi wengine.

Mikutano hiyo ya BBI zimenoga na Jumamosi, Bw Joho akizungumza katika harusi moja akiwa Malindi, Kilifi, aliwasihi viongozi wenzake wa pwani kuwasilisha mambo yote yanayowahusu wapwani ili yajumuishwe katika ripoti hiyo.

Hata hivyo, kufikia sasa Gavana Joho hajatokea hadharani kutangaza mawaziri wapya wala kuzungumzia swala hilo.

Baadhi ya mawaziri waliohudmia kaunti ya Mombasa ni Maryam Mbaruk (Fedha), Godfrey Nato(Mazingira), Hassan Mwamtoa(Ukulima).

Wengine ni Kyalo Munywoki (Vijana), Seth Odongo (Ugatuzi), Fawz Rashid (Utalii), Edward Nyale (Ardhi), Fatma Awale(Maji), Hazel Koitaba (Afya) na Taufiq Balala (Usafiri).

Mawaziri wote kumi walikuwa wakiwahudumia wananchi wa Mombasa kwa miaka miwili mpaka mkataba wao ulipofikia mwisho.

Gavana huyo alitakiwa kutangaza mawaziri wake ili baadaye madiwani waweze kuthibitisha kwenye kikao cha bunge kabla ya wao kuingia ofisini rasmi.

Msemaji wa gavana huyo, Bw Richard Chacha alisema kuwa hajui ni lini mawaziri wapya watatangazwa na Gavana Joho pekee ndiye ataamua muda mwafaka wa kuwatangaza.

“Gavana mwenyewe ataamua ni lini atawatangaza maafisa wake,” alisema Bw Chacha.

Bw Chacha alisema kuwa Gavana hajanyamaza ila ako ziara tofauti ya kikazi.

“Alizuru Kisii na yote ilikuwa kwa ajili ya shughuli muhimu za kikazi,” aliongeza.

Mwaka jana, madiwani walimlaumu Bw Joho wakisema ametumia muda wake mwingi mwaka huu kuzuru ng’ambo na kukosa kikao katika bunge la kaunti.

Wakati huo, alilaumiwa pia kwa kutotoa hotuba yake ya mwaka katika bunge la kaunti, ingawa maafisa wake walidai alikuwa amefanya hivyo awali na kisheria ilihitajika ahutubie bunge hilo mara moja pekee kwa mwaka.

You can share this post!

Kamishna aonya walimu dhidi ya kutoza ada haramu za masomo

Rais, Raila walihofia kuzomewa Kisumu

adminleo