Habari MsetoSiasa

Nzige walivyotafuna kazi ya Kiunjuri

January 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na VALENTINE OBARA

RAIS Uhuru Kenyatta hatimaye ameanza kuwatia adabu viongozi serikalini ambao wanaenda kinyume na amri yake ya kuzima siasa za mapema.

Wadadisi wa kisiasa wanasema kwamba, uamuzi wa Rais kumsimamisha kazi Bw Mwangi Kiunjuri ambaye hadi Jumanne alikuwa Waziri wa Kilimo aliyelemewa kukabiliana nzige waharibifu, ni onyo kwa maafisa wengine serikalini wasiofuata misimamo ya serikali kuu anayosimamia.

Bw Kiunjuri amesimamishwa kazi wakati ambapo joto la kisiasa limezidi nchini kutokana na mgawanyiko uliosababishwa na hatua ya Rais kuongeza muda wa vikao vya jopo la maridhiano (BBI).

Bw Kiunjuri ambaye aliajiriwa katika wadhifa huo mnamo Januari 26, 2018 ameibuka kuwa mmoja wa watetezi wakuu wa Naibu Rais William Ruto katika eneo la Mlima Kenya.

Baadhi ya viongozi katika mrengo wa Tangatanga humtaka awe mgombea mwenza wa Dkt Ruto ifikapo 2022.

“Ni wazi kuwa hatua hii haikosi siasa ndani yake. Inavyoonekana, lengo ni kutoa onyo kwa mrengo wa Ruto kuhusu wanavyopinga misimamo ya serikali kuu,” akasema mchanganuzi wa kisiasa, Bw Holo Oiro.

Maoni sawa na haya yalitolewa na Mbunge wa Suna Mashariki, Bw Junet Mohamed.

“Wale ambao hawana maono sawa na ya Rais Uhuru kupitia kwa handsheki, hawana haja kuendelea kuwa ndani ya serikali yake. Taifa jipya lililo bora zaidi linaundwa,” akasema Bw Mohamed.

Licha ya haya, kuna wadau katika sekta ya kilimo wanaoamini Rais amechukua hatua hiyo kulinda masilahi ya wakulima ambao katika miaka ya hivi majuzi, wamekuwa wakikumbwa na changamoto chungu nzima.

Karibu kila sekta ya kilimo, kama vile kilimo cha miwa, mahindi, majani chai, kahawa na uzalishaji maziwa zimezorota kwa kile ambacho wadau wanasema ni utepetevu na ufisadi katika Wizara ya Kilimo.

Lakini katika kikao cha wanahabari baada ya kumwaga unga, Bw Kiunjuri alisema alitarajia kusimamishwa kazi wakati wowote.

Hata hivyo, alikataa kufafanua ikiwa matarajio hayo yalitokana na misimamo yake ya kisiasa ya kuunga mkono Naibu Rais.

“Sijashangazwa na hatua ya rais. Nashukuru Mungu kwani huu ni mzigo mkubwa ambao nimeondolewa. Nimepitia aibu nyingi na ni Mungu na familia yangu tu wanaoelewa niliyoyapitia. Najivunia mafanikio yangu. Kuanzia sasa, nafungua ukurasa mpya katika maisha yangu kwani Mungu anapofunga mlango mmoja huwa anafungua mwingine,” akasema.

Akazidi kusema: “Nitaendelea kutumikia nchi hii katika nyadhifa zingine. Siendi popote…nitakuwa humu humu.”

Wiki iliyopita, Bw Kiunjuri alijipata lawamani alipoambia Wakenya wapige picha za nzige na kuzituma kupitia mitandao ya kijamii kama njia mojawapo ya Wizara ya Kilimo kukabiliana na wadudu hao waharibifu.

Tangazo hilo lilichukuliwa na wengi kuwa mfano mwingine wa jinsi ameshindwa kutatua matatizo ya wakulima.

Awali, mbunge huyo wa zamani wa Laikipia Mashariki alikuwa Waziri wa Ugatuzi na Mipango kwa miaka miwili katika serikali ya Rais Kenyatta kando na kushikilia nyadhifa nyinginezo katika serikali ya aliyekuwa rais Mwai Kibaki.

Nafasi yake sasa itachukuliwa na Bw Peter Munya, ambaye hadi jana alikuwa ni Waziri wa Biashara na Vyama vya Ushirika.

“Napongeza wakulima kwani wao ndio washindi katika mabadiliko haya ya baraza la mawaziri. Hatua ya Rais kumsimamisha kazi Kiunjuri ilisubiriwa kwa muda mrefu. Amekuwa akisimamia wizara inayotumikia masilahi ya matapeli. Naamini Munya atatimiza matarajio ya Wakenya wote,” akasema Mbunge wa Nandi Hills, Bw Alfred Keter.

Wizara ya Kilimo ambayo ilijumuisha Mifugo na Uvuvi sasa imepewa pia usimamizi wa Vyama vya Ushirika.

Hii ni mara ya tatu Bw Munya, ambaye alikuwa Gavana wa kwanza wa Meru kuhamishwa kwani amewahi pia kuwa Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki.

Bi Betty Chemutai Maina ambaye alikuwa Katibu wa Wizara ya Biashara, ameteuliwa kuchukua mahali pa Bw Munya katika Wizara ya Biashara. Wizara hiyo sasa itaitwa Wizara ya Viwanda, Biashara na Ustawishaji wa Ujasiriamali.

Mwingine aliyeteuliwa kuingia katika Baraza la Mawaziri ni aliyekuwa Seneta wa Nyeri, Bw Mutahi Kagwe ambaye akiidhinishwa na bunge, atakuwa Waziri wa Afya.

Bi Sicily Kariuki aliyesimamia wizara hiyo amehamishwa hadi Wizara ya Maji, Usafi na Unyunyizaji.

Kwa msingi huu, Bw Simon Chelugui aliyekuwa Waziri wa Maji amehamishwa hadi katika Wizara ya Leba ambayo ilikuwa ikisimamiwa na Bw Ukur Yatani.

Rais amemwidhinisha Bw Yatani kuwa Waziri wa Fedha, wadhifa ambao amekuwa akishikilia kama kaimu tangu aliyekuwa waziri Henry Rotich aliposhtakiwa.

Bw Rotich alikana madai mahakamani kuhusu ufisadi wa mabilioni ya pesa katika ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer mwaka uliopita. Hii ni kumaanisha, sasa ni rasmi amemwaga unga.

Mabadiliko mengine ni kwamba Bi Raychelle Omamo amehamishwa kutoka Wizara ya Ulinzi hadi Wizara ya Masuala ya Kigeni. Naye Bi Monica Juma amehamishwa kutoka kwa Wizara ya Masuala ya Kigeni hadi ya Ulinzi.