• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:25 PM
Uhuru atangaza mikakati kufufua kilimo Mlimani

Uhuru atangaza mikakati kufufua kilimo Mlimani

Na WANDERI KAMAU

RAIS Uhuru Kenyatta Jumanne alianzisha harakati za kuzima ghadhabu miongoni mwa wakazi wa eneo la Mlima Kenya kuhusu kuzorota kwa sekta ya kilimo.

Kumekuwa na malalamishi katika eneo hilo, miongoni mwa viongozi na wenyeji kuhusu kudidimia kwa bei za mazao muhimu kama kahawa, majani chai, maziwa, miraa, pareto na mpunga.

Kwa mfano, bei ya wastani ya maziwa katika maeneo mengi ni Sh17, huku wakulima wa majanichai wakipata bonasi ya kiwango cha chini mwaka uliopita ikilinganishwa na miaka ya hapo awali.

Wengi wamekuwa wakiilaumu serikali ya Rais Kenyatta kwa kuitelekeza wizara hiyo muhimu, licha ya kuahidi kuimarisha bei za mazao hayo.

Lakini kwenye hotuba maalum kuhusu mwelekeo wa nchi jana, Bw Kenyatta alitangaza mipango kabambe ya kuimarisha uzalishaji wa mazao hayo, hali inayoonekana kama mbinu za kuwafurahisha wakazi.

Ili kuimarisha sekta ya majanichai, Rais Kenyatta aliiagiza Mamlaka ya Kukadiria Bei za Mazao (CA) kuweka mikakati ya dharura kuhakikisha bei ya majanichai imepanda.

Rais aliiagiza mamlaka hiyo kuhakikisha bei ya majanichai imeongezeka kufikia bei ya wastani ya Sh90 kutoka bei ya sasa, ambapo kilo moja ya majanichai inanunuliwa kati ya Sh41 na Sh50 kwa kilo.

Rais vile vile aliiagiza Wizara ya Kilimo kuanza kutekeleza Kanuni Mpya za Majanichai 2019 ili kuwakabili mawakala ambao wamekuwa wakiwapunja wakulima kwa kununua zao hilo kwa bei ya chini.

“Lazima wizara ianze utelelezaji wa kanuni hizo ili kuhakikisha kila mtu anayeuza majanichai kwa Halmashauri ya Kitaifa ya Kusimamia Majanichai (KTDA) amesajiliwa rasmi kama mkulima wa majanichai,” akasema Rais.

Mbali na hayo, Rais alitoa agizo kwa wizara za Fedha, Biashara na Kilimo kumaliza utekelezaji wa mikakati ya kuimarisha uboreshaji wa majanichai kabla ya kusafirishwa katika masoko ya nje.

Hatua inalenga kuhakisha majanichai ya Kenya yameimarisha ushindani wake katika masoko ya kimataifa.

Kuhusu sekta ya kahawa, Rais aliiagiza Hazina ya Kitaifa kutekeleza Hazina Maalum ya Kahawa, ili kuhakikisha Sh3 bilioni zilizotolewa na serikali kwa wakulima zimewafikia kwa wakati ufaao.

Baadhi ya wakulima katika kaunti za Nyeri, Meru, Murang’a kati ya zingine wamekuwa waking’oa zao hilo wakisema haliwapatii faida.

Na ili kufufua sekta ya maziwa, Rais alitangaza kutenga Sh1.07 bilioni ili kuiboresha sekta hiyo.

Kwenye mkakati huo, serikali inalenga kutumia Sh500 milioni kununua maziwa kutoka kwa wakulima na kuyageuza kuwa unga huku Sh575 milioni zikitumika kununulia mitambo mipya ya kuhifadhi maziwa katika vituo vya Shirika la Kununua Maziwa Kenya (KCC) katika miji ya Nyeri na Nyahururu.

Serikali pia ilieleza mpango wa kuanza kutoza maziwa yoyote kutoka nje kodi ya asilimia 16 ili kuzuia uagizaji wa maziwa ghushi nchini.

Hata hivyo, wadadisi mbalimbali wanasema kuwa namna serikali itakavyotekeleza maagizo hayo ndiyo itaamua ikiwa wenyeji watakumbatia ahadi za Rais Kenyatta.

You can share this post!

Uhuru awapa vijana vyeo vya juu kuwatuliza

Pigo kwa Viusasa na Skiza Tunes serikali ikibadilisha mfumo

adminleo