• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
BBI iandikwe kwa lugha zote za kiasili – Mishra

BBI iandikwe kwa lugha zote za kiasili – Mishra

Na TITUS OMINDE

MBUNGE wa Kesses, Dkt Swarup Mishra ametaka serikali itafsiri Ripoti ya Jopo la Upatanishi (BBI) katika lugha zote za kiasili.

Dkt Kiprop alisema tafsiri ya BBI kwa lugha za kiasili itawawezesha Wakenya zaidi kufahamu yaliyomo kwenye hati hiyo, na kutoa maoni yao kuihusu wakiwa wanaelewa vizuri wanachounga mkono au kupinga wakati wa kura ya maamuzi.

Mbunge huyo alisema kuwa kuna haja ya serikali kutenga fedha ili kufanikisha utafsiri husika.

“BBI ni hati nzuri lakini tunataka itafsiriwe kwa lahaja zote za humu nchini ili kuwezesha Wakenya kutoka jamii zote kuielewa. Ni kupitia hatua hii ambapo wataweza kuyakumbatia yaliyomo kwenye hati hiyo,” alisema Dkt Mishra.

Wito wake unajiri wakati ambapo kumekuwa na pendekezo ripoti hiyo pia itolewe kwa lugha ya Kiswahili.

Wakati wa shughuli ya marekebisho ya Katiba mwaka 2005 na mwaka 2010, kulikuwa na Kielelezo cha Katiba na Katiba rasmi zilizoandikwa kwa Kiingereza na Kiswahili na kusambazwa kupitia magazeti.

Mbunge huyo alishinikiza serikali ijizatiti ili kutekeleza BBI kabla ya mwezi Aprili mwaka huu.

Hata hivyo, aliwaonya wanasiasa dhidi ya kuingiza siasa katika mchakato wa utekelezaji wa BBI.

Mbunge huyo aliwashtumu baadhi ya wanasiasa aliosema wanatumia mjadala wa mapendekezo ya BBI kuleta mgawanyiko serikalini.

Alisema mikutano inayoendelea ya kuunga mkono BBI itaongeza joto la kisiasa nchini.

“Mapendekezo katika BBI ni mazuri na wote tumeyakubali. Hakuna haja ya wanasiasa kuingiza siasa za ubinafsi katika mchakato wa kutekeleza BBI,” akasema.

You can share this post!

Uhuru ahepa swali la ikiwa anaumezea Uwaziri Mkuu

Mbunge amlipia karo mvulana aliyefika shuleni na sabuni...

adminleo