• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 5:39 PM
Teuzi za mawaziri zagawanya jamii ya Wakalenjin

Teuzi za mawaziri zagawanya jamii ya Wakalenjin

Na WAANDISHI WETU

MABADILIKO yaliyotekelezwa kwenye Baraza la Mawaziri na Rais Uhuru Kenyatta majuzi yamegawanya wanasiasa wa jamii ya Kalenjin, baadhi wakidai ni njama ya kuhakikisha ngome ya Naibu Rais Dkt William Ruto haina umoja kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Viongozi kutoka Kaskazini mwa Bonde la Ufa jana walidai mabadiliko hayo yalitunuku nyadhifa mbalimbali watu kutoka maeneo ya Kati, Nyanza na Kusini mwa Bonde la Ufa huku wao wakiachwa nje.

Mnamo Jumanne, Rais Uhuru Kenyatta akiwa katika ikulu ya Mombasa alitangaza mabadiliko ya mawaziri, makatibu na manaibu wa mawaziri huku aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri akipigwa kalamu.

Hata hivyo, kuteuliwa kwa Betty Maina kama Waziri wa Viwanda kumewachemsha nyongo wanasiasa kutoka Kaskazini mwa Bonde la Ufa, wakisema eneo hilo pia lina Waziri wa Kawi Charles Keter ilhali kwao hakuna waziri yeyote.

“Tulimtarajia kiongozi wa nchi kumteua Waziri mwengine kutoka Kaskazini mwa Bonde la Ufa baada ya kutemwa kwa Henry Rotich kama waziri wa fedha. Kama eneo tunahisi kwamba tumetengwa ikizingatiwa eneobunge la Belgut, Bonde la Ufa Kusini sasa lina mawaziri wawili,” akasema Mshirikishi wa Kanu eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa Paul Kibet.

Mshirikishi huyo pia alishangazwa na hatua ya Rais kutomteua mtu yeyote wa chama cha Kanu licha ya urafiki na ushirikiano kati ya Rais na kinara wao Gideon Moi.

Rais Uhuru Kenyatta alimeteua Bi Maina kama Katibu katika wizara ya Afrika Mashariki mnamo 2015 kabla ya kumhamisha hadi wizara za Viwanda na Mazingira mtawalia.

Huku viongozi kutoka Kericho wakiunga uteuzi wa Bi Maina, wenzao kutoka Bomet walisema eneo hilo limeachwa nje ya serikali ikizingatiwa, Kericho itanufaika na uwaziri wa Bw Keter na Bi Maina.

Kwingineko, Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria, amesema kuwa utekelezaji wa ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) hautafaulu iwapo Naibu Rais William Ruto hatahusishwa kikamilifu.

Bw Kuria alisema kwamba kuhusishwa kwa Dkt Ruto sio jambo la kufikiria au kuchagua, mbali ni jambo la lazima ikiwa mchakato huo utazaa matunda.

Dkt Ruto na wandani wake, akiwemo Bw Kuria, wamekuwa wakidai kuwa mikutano ya awamu ya pili ya kujadili ripoti ya BBI ni kuharibu pesa wakisisitiza kuwa hakuna anayepinga ripoti iliyozinduliwa mwaka jana.

Kulingana na Dkt Ruto, mikutano inayoandaliwa ni njama ya chama cha ODM ya kupanga jinsi kitashinda uchaguzi mkuu wa 2022 na wanasiasa kupanga watakavyogawana mamlaka kwa kubuni nafasi mpya serikalini.

Kwenye taarifa baada ya hotuba ya Rais kwa taifa Jumanne, Bw Kuria alisema japo Rais alitangaza hatua za kufanikisha BBI, hazitaweza kufaulu ikiwa Naibu Rais William Ruto hatahusishwa na kuheshimiwa.

“Kuhusu mchakato wa BBI na mazingira ya kisiasa ya kuitekeleza, hatua alizotangaza ( Rais Kenyatta) zinafaa. Cha kuongeza ni kuwa, kila mmoja anapaswa kufahamu kwamba ili BBI iweze kufaulu, kuhusika, kushiriki na kuheshimiwa kwa Naibu Rais ni suala la lazima. Sio chaguo,” Bw Kuria alisema.

Kulingana na mbunge huyo mbishi, ikiwa Dkt Ruto atahusishwa, BBI haitafaulu. BBI ilifuatia handisheki kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga na Dkt Ruto hakuhusishwa.

Ripoti za Benson Matheka, Barnabas Bii Na Wycliff Kipsang

You can share this post!

Maisha yangu yamo hatarini – Alice Wahome

Viongozi wamsifu Rais Kenyatta kuteua Munya Waziri wa Kilimo

adminleo