• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
Hofu Marekani ikipunguza ufadhili nchini

Hofu Marekani ikipunguza ufadhili nchini

Na RUTH MBULA

BALOZI wa Marekani nchini Kyle McCarter ametangaza kwamba serikali yake inaendelea kupunguza msaada wa kifedha kwa Kenya na kuhimiza ushirikiano wa kibiashara ili kufanikisha ukuaji wa kiuchumi.

Bw McCarter alisema anaamini Kenya ni taifa ambalo halifai kutegemea misaada na badala yake linafaa kuwa kielelezo bora kwa mengine kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Kauli ya balozi huyo inajiri huku kukiwa na sintofahamu kwamba Marekani imepunguza ufadhili wake kwa miradi muhimu jambo ambalo limeathiri hali ya maisha ya raia.

“Tuna nia ya kupunguza msaada na kukumbatia biashara. Hiyo inamaanisha kwamba tutaimarisha uwekezaji ili kuwasaidia wakulima kuimarisha mapato yao,” akasema akiwa kwenye ziara Kaunti ya Kisii.

Balozi huyo kwa muda wa miezi michache iliyopita, amekuwa akitembelea kaunti mbalimbali, Kisii ikiwa ya 32 na ameahidi kwamba atatembelea magatuzi yote 47.

“Ni vyema kwamba Marekani isiwakilishwe tu Nairobi lakini kwa kila kaunti. Ni vyema tufahamiane ili tusaidiane. Tunapigia upatu urafiki. Marafiki ambao husaidiana,” akasema.

Bw McCarter alitembelea Hospitali ya Rufaa ya Kisii ambapo alikagua miradi ya maendeleo huku akisema mfumo wa ugatuzi umesaidia sana kwenye uimarishaji wa maisha ya raia. Pia alimsifu Gavana James Ongwae kwa kusaidia katika uimarishaji wa sekta ya afya.

“Gavana amekuwa akifikiria na kuwajibika. Ana maono makubwa kwa watu ambao amekuwa akiwawakilisha na amekuwa akiwapigania wanaufaikie miradi ya serikali,” akasema.

Bw Ongwae naye alisifu mchango wa Marekani nchini, akisema anaomba taifa hilo lisaidie Kenya kuimarisha sekta ya afya na kukabiliana na majanga.

You can share this post!

Wakuzaji kahawa Kirinyaga kufaidi ushirikiano na India

Nafasi za kazi kwa wanaosaka ajira

adminleo