Habari Mseto

Kesi ya Sonko kuendelea

January 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na Richard Munguti

GAVANA Mike Sonko Alhamisi alipata pigo kubwa Mahakama kuu ilipokataa kusitisha kusikizwa kwa kesi ya ufujaji wa zaidi ya Sh357milioni pesa za umma.

Jaji Mumbi Ngugi alikataa kuamuru mahakama ya kuamua kesi za ufisadi isiendelee kusikiza mashtaka zaidi ya 30 dhidi ya Sonko.

Jaji Ngugi aliamuru mawakili Cecil Miller na George Kithi wakabidhi nakala za kesi hiyo tume ya kupambana na ufisadi (EACC) ijibu madai kwamba ilikosea kumfungulia mashtaka ilhali mmoja wa maafisa wake wakuu wa uchunguzi na upelelezi anadaiwa na Sonko alihusika na ufisadi.

Katika ombi lake Bw Sonko amedai mkurugenzi wa uchunguzi EACC Bw Abdi Mohamud alihusika na uuzaji wa jumba la Integrity Centre kwa zaidi ya Sh1.5bn na kunyakua uwanja wa shule.

Bw Sonko alidai kwamba EACC haipasi kumchunguza kwa vile kinara wake amehusishwa na unyakuzi wa uwanja wa shule moja ya msingi na uuzaji kwa njia ya ufisadi Integrity Centre akishirikiana na watu wengine.