• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:27 PM
Makabiliano makali yanukia Nakuru

Makabiliano makali yanukia Nakuru

Na JOSEPH OPENDA

MAKABILIANO makali ya kisiasa yamechipuka katika Kaunti ya Nakuru, baada ya wabunge wa ‘TangaTanga’ kumlaumu Gavana Lee Kinyanjui kwa masaibu yanayowakumba.

Makabiliano hayo yalichipuza baada ya Seneta Susan Kihika na mbunge David Gikaria (Nakuru Mjini Mashariki) kuzuiwa kuhudhuria hafla ya Rais Uhuru Kenyatta.

Hafla hiyo ilihusu utoaji wa hatimiliki za ardhi kwa wakazi wa kaunti ndogo za Njoro, Bahati, Subukia na Gilgil.

Wabunge hao sasa wanamlaumu Bw Kinyanjui kwa kupanga njama hiyo na maafisa wa utawala wa mkoa, ili kuwahangaisha. Wanadai Gavana ni wa mrengo wa ‘Kieleweke’.

Bi Kihika alisema Gavana Kinyanjui alihofia uwepo wao ndiposa akaamua kugeuza hafla hiyo kuwa jukwaa la kisiasa. Seneta Kihika analenga kuwania ugavana mwaka 2022.

“Yaliyofanyika hayahusiani kwa vyovyote vile na uwepo wa Rais Kenyatta. Tunajua kuna watu walitishiwa na uwepo wetu wakaamua kutuhangaisha bure,” akasema Bi Kihika.

Kwa upande wake, mbunge wa Nakuru Mjini Mashariki alimlaumu Gavana Kinyanjui kwa kukosa kuwaheshimu viongozi waliochaguliwa na wananchi.

Bw Gikaria alisema kuwa ni viongozi hao waliochangia pakubwa kwa Rais Kenyatta kuchaguliwa tena.

“Naamini kwamba viongozi wa eneo hili, wakiongozwa na Gavana pamoja na Kamishna wa Kaunti, Bw Erastus Mbui walihusika kusababisha masaibu yaliyotukumba. Kama viongozi, tunamheshimu sana Rais kwani ndiye ishara ya umoja miongoni mwetu,” alieleza.

You can share this post!

EU yamuunga mkono Rais wafisadi waadhibiwe vikali

Wakulima wa mahindi watoa masharti makali kwa serikali

adminleo