Habari Mseto

Wakulima wa mahindi watoa masharti makali kwa serikali

January 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na BARNABAS BII

WAKULIMA wa mahindi katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa wametoa masharti makali kwa serikali kabla ya kuiuzia mazao yao baada ya wasagaji kuahidi kununua zao hilo kwa bei za juu.

Hali imechangiwa na upungufu wa zao hilo unaotarajiwa kuyakumba maeneo mengi nchini baadaye mwakani.

Wakulima hao sasa wanaitaka serikali kununua gunia moja kwa Sh4,000 kwenda juu kutoka bei ya Sh2,500 mwaka uliopita.

Wakulima pia wanaitaka serikali kupunguza masharti makali ambayo imewawekea wanapowasilisha mahindi yao kwa Halmashauri ya Kitaifa ya Ununuzi wa Nafaka (NCPB).

Wamepinga vikali pendekezo la serikali kuwalipa baada ya kuwasilisha mazao yao kwa halmashauri hiyo.

“Tunaitaka serikali kununua mazao yetu kwa bei nzuri; pengine Sh4,000 kwa gunia moja la kilo 90 kwenda juu. Lazima pia itulipe mara moja baada ya kuwasilisha mazao yetu,” akasema Bw Isaac Kosgey kutoka eneo la Moiben, Kaunti ya Uasin Gishu.

Halmashauri ya Maghala Maalum ya Kuhifadhi Vyakula (SFR) imetenga Sh10 bilioni za kununua mahindi msimu huu.

Halmashauri hiyo inakumbwa na ushindani mkali kutoka kwa wasagaji, wanaonunua mahindi hayo kwa bei ya juu.

Jana, wasimamizi wa maghala hayo walisema kwamba, watanunua mazao hayo kwa bei ya chini ya Sh3,200 ambayo ndiyo bei ya wastani wasagaji wananunua mahindi kwayo.

“Bado hatujatangaza bei tutakayoyanunua mahindi kwayo. Hata hivyo, itakuwa chini ya kiwango kinachotolewa na wasagaji,” akasema Dkt Noah Wekesa, ambaye ndiye mwenyekiti wa halmashauri hiyo.