'Wazir kipenzi cha wabunge wanawake si mwendawazimu' – Ripoti
Na RICHARD MUNGUTI
MWANAUME anayedaiwa kuwa kipenzi cha wabunge wanawake na aliyetumia jina la mbunge mwakilishi wa wanawake kaunti ya Murang’a Bi Sabina Wanjiru Chege sio mwendawazimu.
Ripoti iliyotolewa Jumanne na hospitali ya Mathare inasema kwamba “Wazir Benson Masubo Chacha yuko na akili timamu.”
Wazir (pichani) alipimwa na Dkt Mercy Karanja wa hospitali ya Mathare baada ya wakili Job Ngeresa anayemtetea kudai Waziri alikuwa “ na akili isiyo timamu”
Bw Ngeresa alimsihi hakimu mkazi Bi Christine Njagi aamuru polisi wampeleke Waziri hospitali ya Mathare mnamo Aprili 9, 2018 kupimwa akili na ripoti iwasilishwe.
Maafisa wawili wa polisi walimpeleka Chacha kwa Dkt Karanja aliyempima akili ndipo akasema , “mshtakiwa hakuwa na tabia mbaya na alikuwa na anazugumza kwa njia laini.”
Dkt Karanja aliongeza kusema , “Chacha ni mwadilifu na hajawahi patwa na wazimu na anakumbuka masuala yote ya maisha yake kwa njia barabara. Anajua masuala yote ya kesi inayomuhusu na yuko tayari kujitetea.”
Dkt Karanja alisema mshtakiwa ni mchangamvu na “ hana historia yoyote ya kutibiwa ugonjwa wa akili.”
Bw Ngeresa anayemtetea mshtakiwa pamoja na wakili Edwin Saluny alieleza mahakama kwamba mshtakiwa aliyetiwa nguvuni mjini Tarime nchini Tanzania na kudaiwa alikuwa akijaribu kutorokea nchini Congo alikuwa anaenda kupokea matibabu ya ubongo katika hospitali ya Muimbili iliyoko Tanzania.
Bw Saluny alimweleza hakimu mkuu Bi Roseline Oganyo kwamba mshtakiwa mwenye umri wa miaka 25 anatoka kijiji cha Masaba ambacho ni kilomita 15 kutoka mji wa Tarime.