Habari MsetoSiasa

Presha Duale na Murkomen watimuliwe yazidi

January 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na ONYANGO K’ONYANGO

SHINIKIZO imezidi kutolewa kwa Chama cha Jubilee kubadilisha viongozi wa wengi na viranja katika bunge la taifa na seneti, ikisemekana hawaheshimu misimamo ya Rais Uhuru Kenyatta aliye pia kiongozi wa chama.

Mnamo Jumamosi, katika mkutano wa mashauriano wa BBI katika uwanja wa Bukhungu, Kaunti ya Kakamega, Mbunge Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Wajir Fatuma Gedi alijiunga na mjadala wa kutaka Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Taifa Aden Duale na mwenzake wa Seneti, Bw Kipchumba Murkomen watimuliwe.

Duru zimesema viongozi wandani wa Rais Kenyatta, wakiwemo wabunge Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini), Joshua Kutuny (Cherang’any), Amos Kimunya (Kipipiri), Paul Koinange (Kiambaa) na Muturi Kigano wa Kangema wanatazamiwa kusimamia mchakato wa kuwaondoa viongozi hao.

Viranja wanaolengwa ni Benjamin Washiali wa bunge la taifa na Susan Kihika wa seneti.

Jana, Bw Kutuny alisema wanachama wa Jubilee hawataenda kwenye chaguzi za chama ikiwa uongozi wa nyumba zote mbili za bunge hazitafanyiwa mabadiliko kwani viongozi hao wamekuwa vizingiti kwenye ajenda za Rais.

“Baada ya baraza la mawaziri kubadilishwa, sasa tunaweka misingi ya kuwaondoa walio katika nafasi kuu ndani ya chama chetu na wanapinga miradi ya Rais kama BBI,” akasema.

Lakini wandani wa Dkt Ruto walipuuzilia mbali vitisho hivyo.

Wakiongozwa na Mbunge wa Keiyo Kusini Daniel Rono, wanasiasa hao wa mrengo wa Tangatanga walisema watasambaratisha shughuli bungeni kama wenzao watachukua hatua hiyo.

Mbunge wa Aldai Cornelius Serem alisema Chama cha Jubilee hakijashindwa kufanya kazi ipasavyo kwa hivyo hakuna haja ya kuanzisha mipango aina hiyo kwani haitafua dafu.