• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Babu Owino ndani siku 7

Babu Owino ndani siku 7

Na RICHARD MUNGUTI

MBUNGE wa Embakasi Mashariki Paul Ongili almaarufu Babu Owino anakondolewa macho na kifungo cha maisha gerezani akipatikana na hatia katika kesi inayomkabili ya kujaribu kumuua DJ katika kilabu kimoja jijini Nairobi siku nne zilizopita.

Na wakati huo huo hakimu mkuu mahakama ya Milimani Nairobi Bw Francis Andayi aliamuru Bw Owino azuiliwe katika gereza la Viwandani kwa muda wa siku saba kuwezesha idara ya urekebishaji tabia kumhoji mhasiriwa Felix Odhiambo Orinda.

Bw Andayi ataamua ikiwa atamwachilia mbunge huyo wa dhamana kulingana na jinsi Bw Orinda, anayeendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Nairobi Hospital atakavyosema.

Hakimu alisema ni muhimu Bw Orinda kueleza ikiwa anahofia maisha yake au la kabla ya mahakama kutoa uamuzi ikiwa “itamwachilia kwa dhamana Bw Owino.”

Pia maafisa kutoka idara hiyo ya kurekebisha tabia itamhoji Bw Owino kutoka gerezani “kuelezea masuala kadhaa kumuhusu.”

Hakimu mkuu Francis Andayi. Picha/ Richard Munguti

Bw Andayi aliamuru Bw Owino azuiliwe katika gereza la Viwandani baada ya kiongozi wa mashtaka Bw Jacob Ondari kupinga akiachiliwa kwa dhamana.

Bw Ondari alisema upande wa mashtaka unahofia mshtakiwa atavuruga mashahidi ikitiliwa maanani “umaarufu wake kisiasa.”

“Mshtakiwa alijaribu kumshawishi baba yake mlalamishi jambo ambalo limefanya wachunguzi kuhofia atawavuruga mashahidi,” hakimu alifahamishwa.

Bw Ondari alisema mlalamishi yuko katika hali mbaya licha ya kuwa anaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Nairobi Hospital.

Mahakama ilielezwa kuwa mashahidi wanaotegemewa watatoka B Club ambapo tukio hilo lilitendeka.

“ Jaribio la Bw Owino kujaribu kumfikia baba yake mlalamishi ni sababu tosha atawavuruga mashahidi. Naomba hii mahakama isimwachilie kwa dhamana kwa sababu ya manufaa ya umma,” alisema Bw Ondari.

Kiongozi huyo wa mashtaka alisema kuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha Bw Owino alinuia kusababisha kifo cha Bw Orinda.

“Naomba mahakama isimwachilie mshtakiwa kwa dhamana kwa vile atatoroka.Adhabu ya makosa aliyofanya ni kifungo cha maisha gerezani,” Bw Ondari.

Lakini mawakili Cliff Ombeta, Dunstan Omari na Duncan Okatchi waliomba korti imwachilie mshtakiwa kwa dhamana “ kwa vile ni haki yake ya kikatiba.”

Wakili Dunstan Omari (kati) anayemwakilisha Owino. Picha/ Richard Munguti

Bw Ombeta alisema Bw Owino amelipa gharama ya hospitali Sh600,000.

Alisema madai ya DPP kwamba mshtakiwa atawavuruga mashahidi ni uvumi mtupu.

“Hakuna ushahidi wowote uliowasilishwa na Bw Ondari kuthibitisha mshtakiwa atawavuruga mashahidi,” Bw Ombeta.

Mahakama ilielezwa baada ya kisa hicho, Bw Owino alimpeleka mlalamishi hospitali.

Bw Ombeta alisema kitendo hicho cha mshtakiwa ni ishara ya utu wema.

Mawakili waliomba mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana kwa vile hawezi kutoroka.

“ Mshtakiwa ameoa na yuko na watoto watatu wenye umri wa miaka tisa , miaka minne na mwaka mmoja. Anategemewa na familia yake,” Bw Ombeta alisema.

You can share this post!

Ulinzi Youth na Falling Waters majogoo wa Mlima Kenya

Machifu, wahubiri walaumiwa kwa mauaji ya wazee

adminleo