Yaibuka magavana walifuja pesa kufadhili BBI
Na SHABAN MAKOKHA
MADIWANI kutoka kaunti za kanda ya Magharibi wamewataka magavana kuelezea walikotoa fedha walizotumia kusafirisha wafuasi wao hadi kwenye mkutano wa kupigia debe ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) katika uwanja wa Bukhungu mjini Kakamega, Jumamosi iliyopita.
Madiwani hao kutoka Kaunti za Kakamega na Vihiga, walisema kuwa mabunge ya kaunti hayakutenga fedha kwa ajili ya BBI.
Madiwani wa Bunge la Kaunti ya Kakamega Kelvin Mahelo (Butali-Chegulo), Roselida Adamba (Maalumu) na mwenzao wa Vihiga Jackline Mwenesi waliitaka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na Idara ya Kuchunguzi Uhalifu (DCI) kuchunguza chanzo cha fedha zilizotumiwa kusafirisha wafuasi wa magavana hadi Bukhungu.
Madiwani hao wanashuku kwamba huenda viongozi wa kaunti za Magharibi walitumia fedha za umma kusafirisha wafuasi wao.
Bw Mahelo alidai kuwa kila mtu aliyehudhuria mkutano huo alilipwa Sh5,000.
“Baadhi ya vijana walitakiwa kuhudhuria mkutano huo na wakaahidiwa kulipwa Sh5000 kila mmoja. Lakini mkutano ulipoisha waliachwa bila kupewa fedha walizoahidiwa,” akadai Bw Mahelo.
Aliyekuwa Seneta wa Kakamega, Boni Khalwale alidai kuwa magavana wa Trans Nzoia, Bungoma, Busia, Kakamega na Vihiga walifadhili mkutano wa Bukhungu.
“Serikali ya Kaunti ya Kakamega ilitoa Sh100 milioni kwa ajili ya mkutano uliofanyika Jumamosi uwanjani Bukhungu. Kaunti za Trans Nzoia na Vihiga zilitoa Sh15 milioni kila moja. Kaunti za Bungoma na Busia zilichanga Sh30 milioni kila moja,” akadai Dkt Khalwale.
Lakini Gavana Wycliffe Oparanya wa Kakamega alipuuzilia mbali madai hayo akisema kuwa ripoti ya BBI ni ya kitaifa na mikutano hiyo imefadhiliwa na jopo la BBI lililoteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta.