Simba waliolemewa na njaa wapata ufadhili wa chakula
Na AFP
KHARTOUM, Sudan
MSAADA wa nyama unazidi kumiminika katika hifadhi ya wanyamapori nchini Sudan inayokabiliwa na uhaba wa hela huku simba wa kiume na simba jike wakizidiwa na njaa.
Picha za wanyamamwitu hao katika Mbuga ya Wanyamapori ya Al-Qureshi jijini Kahrtoum, zilienezwa mitandaoni baada ya mwanaharakati Osman Salih kuzichapisha.
Wanyama hao walisalia ngozi na mifupa tu na walihitaji matibabu.
Salih alisema wafadhili walitoa “nyama nyingi” na kondoo wawili ili kuwalisha wanyama hao.
Mpango wa kupata nyama kila wakati kutoka vichinjioni na viwanda nchini humo pia uliafikiwa.
Kulingana na wafanyakazi, baadhi ya wanyama walipoteza karibu thuluthi mbili ya uzani wa miili yao katika majuma ya hivi majuzi kutokana na ukosefu wa chakula na dawa, hali ambayo imesababishwa na matatizo ya kiuchumi nchini humo.
Msimamizi wa mbuga hiyo Brigadier Essamelddine Hajjar, alieleza vyombo vya habari kuwa, baadhi ya wafanyakazi hata walitumia hela zao binafsi kuwanunulia chakula wanyama hao.
Salih ambaye amekuwa akitoa habari kuhusu jinsi wanyama hao wanavyoendelea alitangaza kuwa mmoja alikuwa amefariki.
“Nasikitika kuwafahamisha kwamba simba jike aliyekuwa mgonjwa amefariki. Jana daktari aliwapa matibabu simba jike wawili waliokuwa wagonjwa ambapo baadaye aliwapa chakula. Mmoja alipata nafuu lakini mwingine akafariki. Sasa tunachunguza kiini cha kifo.”
Tafsiri imefanywa na MARY WANGARI