• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Oloo atetea vikao vya BBI akisema ni vya uhamasisho

Oloo atetea vikao vya BBI akisema ni vya uhamasisho

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA naibu mwenyekiti wa jopo kazi la maridhiano (BBI) Adams Oloo, ametetea msusururu wa mikutano ya uhamasisho kuhusu ripoti yao akisema ni sehemu ya mdahalo wa kitaifa kuhusu ripoti yenyewe.

Dkt Oloo alisema aya ya 23 katika utangulizi wa ripoti iliyozinduliwa rasmi mnamo Novemba 27 mwaka jana, inapendekeza kuwa viongozi wa matabaka mbalimbali kuandaa mdahalo huo ili kutoa nafasi kwa wananchi kuzungumzia ripoti hiyo.

Aliongeza kuwa Sura ya 12 ya ripoti hiyo pia inawataka viongozi mbalimbali nchini “kuivumisha ripoti hiyo ili imilikiwe na Wakenya”.

“Midahalo hiyo inapasa kuendeshwa katika katika makanisa, misikiti, kumbi za miji, katika mikutano ya vyama vya kisiasa miongoni mwa majukwaa mengine. Na mikutano hii inaweza kuandaliwa na viongozi wa kidini, wanasiasa, makundi ya mashirika ya umma, vyama vya wafanyakazi na makundi mengine ya kijamii,” akasema Jumatutu usiku akihojiwa na wanahabari wa runinga ya KTN.

Dkt Oloo alisema ni katika mikutano kama hiyo ambapo wananchi na viongozi wanapaswa kuchambua na kudadisi ripoti hiyo kisha kupendekeza sehemu ambazo zinapasa kufanyiwa marekebisho.

“Lakini mijadala hiyo inapasa kujikita katika mada tisa ambazo tulishughulikia tulipokuwa tukizunguka kote nchini kukusanya maoni ya Wakenya wala sio siasa za 2022,” akasema. Mada hizo ni kama vile; ukabila, vita dhidi ya ufisadi, ukosefu wa maadili ya kitaifa, usalama, ujumuishaji wa wote katika teuzi za serikali, kuboreshwa ugatuzi na chaguzi zinazoleta migawanyiko.

Naibu Rais William Ruto amepuuzilia mbali mikutano ya uhamasisho kuhusu ripoti ya BBI iliyofanyika mijini Kisii na Kakamega akidai iligeuzwa majukwaa ya wanasiasa kuchapa siasa za 2022.

Akiongea Jumapili katika kaunti ya Machakos, Dkt Ruto alitoa wito kwa wanachama wa jopo la BBI kutoa ratiba kuhusu mikutano ya kukusanya maoni zaidi kutoka kwa Wakenya ili “mchakato huo usitekwe nyara na wanasiasa wanaojitakia makuu.”

“Ripoti ya BBI ilipotolewa, Rais Uhuru Kenyatta aliagiza nakala za kutosha zitolewe na zisambaziwe Wakenya ili wasome na kujiamulia. Kwa nini sasa wanasiasa wengine wamejitwika wajibu wa kuwasomea wananchi ripoti hiyo katika mikutano ya kisiasa?,” Dkt Ruto akauliza Jumapili alipohudhuria ibada Machakos Mjini.

Alisema mikutano iliyoandaliwa Kisii na Kakamega ilisheheni “sarakasi” na siasa za kumharibia jina badala ya masuala yenye umuhimu kwa Wakenya kuhusu BBI.

Japo Dkt Oloo alikubaliana na kauli ya Dkt Ruto kwamba baadhi ya viongozi wa kisiasa waligeuza mikutano hiyo kama majukwaa ya kuchapa siasa, alisema mapendekezo muhimu kuhusu mada tisa za BBI yaliyosomwa kwa hadhara.

You can share this post!

Tangatanga sasa wakubali kueneza injili ya BBI kote nchini

Jaji Mumbi ajiondoa kwa kesi ya Sonko

adminleo