• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Jaji Mumbi ajiondoa kwa kesi ya Sonko

Jaji Mumbi ajiondoa kwa kesi ya Sonko

RICHARD MUNGUTI na LUCY MKANYIKA

JAJI Mumbi Ngugi wa Mahakama Kuu , amejiondoa katika kesi ya ufisadi dhidi ya Gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko.

Hayo yalijiri huku gavana huyo akitarajia uamuzi leo iwapo ataondolewa mashtaka dhidi yake katika mahakama ya Voi, kaunti ya Taita-Taveta.

Jaji Ngugi alijiondoa katika kesi ambayo Bw Sonko anaomba kesi ya ufisadi wa Sh357milioni ifutiliwe mbali.

Katika kesi hiyo pia Bw Sonko anaomba majaji watatu, Jaji Ngugi , Jaji Ngenye Macharia na Jaji John Onyiengo wajiondoe katika kesi hiyo.

Bw Sonko pia anaomba kesi hiyo iwasilishwe mbele ya Jaji Mkuu David Maraga ateue jopo la kuamua iwapo masharti ya dhamana ya hakimu yanaweza kumzuia kutekeleza majukumu yake ya Ugavana kaunti ya Nairobi.

Katika mahakama ya Voi kaunti ya Taita Taveta, Kamanda wa Polisi ukanda wa Pwani, Bw Rashid Yakub aliomba mahakama ifutilie mbali kesi dhidi ya Bw Sonko kwa vile “hataki kuendelea na kesi dhidi ya Sonko.”

Bw Sonko alikuwa amefika mahakama ya Voi kujibu mashtaka matatu ya kumjeruhi Bw Yakub, kuzuia kukamatwa kwake na kuwa na tabia ya kuudhi.

Alishtakiwa kutekeleza makosa hayo Desemba 6, 2019.

Akiwasilisha ombi hilo mbele ya Hakimu Mkuu wa mahakama ya Voi, Bw Fredrick Nyakundi, naibu wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Bw Alois Kemo alisema “mlalamishi hataki kuendelea na kesi hiyo.”

Hata hivyo, mahakama haikuarifiwa sababu za mlalamishi kutaka kuondoa kesi hiyo.

Wakili wa Bw Sonko, Bw Cecil Miller alisema kuwa gavana huyo hakuwa na pingamizi kuhusu kuondolewa kwa mashtaka dhidi yake.

“Hatuna pingamizi yoyote kuhusu ombi lililowasilishwa na kiongozi wa mashtaka,” akasema Bw Miller.

Mahakama itatoa uamuzi leo iwapo itafutilia mbali kesi hiyo au la.

“Nitatoa uamuzi kuhusu ombi hili kesho (leo),” akasema Bw Nyakundi.

Awali, maafisa wa usalama walishika doria na kuweka vizuizi vya barabarani katika maeneo ya mahakama hiyo ili kuzuia umati uliokuwa umewasili kushuhudia kesi hiyo.

Maafisa hao walikuwa na wakati mgumu kuwazuia wafuasi wa gavana huyo waliotaka kuingia kortini. Baadhi ya waliohudhuria kesi hiyo ni aliyekuwa mbunge wa Kibwezi Magharibi, Bw Kalembe Ndile.

You can share this post!

Oloo atetea vikao vya BBI akisema ni vya uhamasisho

Ngilu azindua ambulansi 10 kusaidia wagonjwa mahututi

adminleo