• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 11:05 AM
Uhamisho wa walimu walemaza masomo

Uhamisho wa walimu walemaza masomo

Na BRUHAN MAKONG

SHULE katika eneo la Kaskazini mwa Kenya zinakabiliwa na wakati mgumu kuendesha masomo, baada ya Wizara ya Elimu kuhamisha walimu kufuatia visa vya mashambulizi ya kigaidi.

Mwakilishi wa Chama cha Walimu (KNUT) tawi la Wajir, Bw Mohamed Bardad alieleza Taifa Leo kuwa, shule nyingi katika maeneo ya Wajir Kusini, Mashariki na Tarbaj ziliathirika zaidi kutokana na uhamisho huo.

Sasa baadhi ya taasisi hizo ziko katika hatari ya kufungwa.

Kwa mfano, katika eneobunge la Wajir Kusini, walimu 47 walihamishwa.

Shule zilizopoteza walimu wengi zaidi ni ile ya msingi na upili ya Dadajabula, za msingi za Biyamadhow, Sarif na Sala.

Katika eneo la Tarbaj, walimu 45 walihamishwa. Bw Bardad alisema kuwa shule katika wadi za Wargadud, Kutulo na Lafaley zinaelekea kufungwa kutokana na ukosefu wa walimu.

Kati ya wadi nne za eneo la Tarbaj, ni moja tu- Sarman, ambayo imeorodheshwa kuwa salama kwa walimu.

Shule za upili na msingi za Elben, Qajaja, Dasheq na Mansa pia ni miongoni mwa zile zilizopoteza walimu wengi zaidi.

Katika eneo la Wajir Mashariki, walimu 24 walihamishwa, hatua iliyoacha hali ya masomo ikiwa tete.

Huko Garissa, walimu ambao wamekuwa wakifanya kazi maeneo ya mpakani mwa Kenya na Somalia tayari wamehamishiwa shule zingine zilizo katika maeneo salama.

Hatua hiyo iliathiri shule za kaunti nne ndogo za Fafi, Dadaab, Ijara na Hulugho.

Idadi ya walimu ambao wamehamishwa kutoka Kaunti ya Mandera, hata hivyo, haijulikani japo idadi kubwa ya shule zimeachwa bila walimu wa kutosha.

Ijumaa iliyopita Rais Uhuru Kenyatta aliahidi kwamba, serikali itaimarisha vita dhidi ya magaidi wa Al-Shabaab ambao wamekuwa wakitekeleza mashambulizi kiholela katika maeneo ya Kaskazini Mashariki na Pwani, hususan wakati muhula wa kwanza ulipofunguliwa majuma machache yaliyopita.

Hata hivyo, Bw Bardad asema hiyo haitakuwa suluhisho kwa matatizo yanayokumba sekta ya elimu eneo hilo.

Alisema kinachohitajika ni kutafuta mbinu mwafaka itakayoleta mabadiliko ya kudumu.

Mwakilishi huyo wa Knut alitaja pendekezo la aliyekuwa Waziri wa Elimu Amina Mohammed (sasa Waziri wa Michezo) kwamba, gredi ya wanaotaka kusomea ualimu kutoka eneo hilo ipunguzwe.

Alipigia upatu kauli hiyo kwamba ingekuwa suluhu bora kwa matatizo hayo ya ukosefu wa walimu wa kutosha eneo la Kaskazini Mashariki.

Pendekezo hilo lilikataliwa na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC).

“Ikiwa wanafunzi waliokuwa wameteuliwa kwa mafunzo ya ualimu chini ya mfumo huo hawangetimuliwa chuoni, pengine hatungekuwa na matatizo sugu kiasi hiki,” akaeleza.

You can share this post!

Nzige sasa waharibu mimea Baringo na Turkana

Afokea pasta kwa kumkataza kuoa kidosho

adminleo