Habari MsetoSiasa

Ngunjiri asalimisha bunduki yake kwa polisi

January 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

ERICK MATARA NA RICHARD MAOSI

Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri Jumanne alisalimisha bunduki yake katika makao makuu ya DCI Nakuru baada ya maafisa wake wote wa ulinzi kuondolewa na serikali.

Leseni ya kumiliki bunduki pia ilifutiliwa mbali, ikiaminika kuwa hii ni njia mojawapo ya kuwahangaisha wandani wa naibu rais Dkt William Ruto.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali Bw Ngunjiri alisema masaibu yake yalianza baada ya kutoa maoni yake kuhusu jinsi naibu rais alivyofurushwa kutoka kwenye makao yake mjini Mombasa.

Alieleza kuwa baadhi ya watu wenye ushawishi mkubwa serikalini, walikuwa na njama ya kumhangaisha naibu rais.

Kamanda wa polisi kutoka kaunti ya Nakuru Stephen Matu alithibitishahabari hizo akisema kuwa Bw Ngunjiri alikuwa amesalimisha silaha yake kwa DCI , isipokuwa hakuwa na uhakika endapo ni matamshi aliyotoa kumtetea naibu wa rais ndiyo yalimtia mashakani.

Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri afika kwenye makao ya makuu ya DCI Nakuru kusalimisha bunduki yake. Picha/Richard Maosi

“Ni kweli mbunge wa Bahati amesalimisha silaha yake kama agizo lilivyotolewa siku ya Jumatatu,” akasema.

Hata hivyo mmoja wa makachero wakuu alisema Ngunjiri aliandikisha taarifa kuhusiana na matamshi aliyokuwa ametoa kuhusu naibu rais siku ya Jumatatu.

“Bw Ngunjiri aliandikisha taarifa Jumatatu lakini Jumanne pia alilazimika kufika mbele ya DCI,” Matu aliongezea akisema kuwa alipokonywa silaha yake kwa sababu uchunguzi kuhusu matamshi yake ulikuwa ukiendelea.

Hapo Jumatatu Bw Ngunjiri alifika katika makao ya DCI mwendo wa saa tatu asubuhi na kufanyiwa mahojiano kwa zaidi ya saa moja.

Akizungumza katika makao ya DCI, muda mfupi baada ya kusalimisha silaha yake, alisema hatayumbishwa na chochote kwa kumuunga naibu rais mkono.

Bw Ngunjiri akiwa na wafuasi wake baada ya kusalimisha bunduki. Picha/Richard Maosi

“Ninafahamu nimepokonywa bunduki yangu pamoja na maafisa wangu wa usalama kuamuriwa warudi Nairobi, hii ni katika mojawapo ya njama za kuninyamazisha kisiasa,”akasema.

Alimlaumu waziri wa usalama wa ndani Dkt Fred Matiang’i kwa kuwazima wale wanaounga mkono mrengo wa naibu rais.

Bw Ngunjiri anahitimisha idadi ya viongozi sita ambao kufikia sasa wamepokonywa silaha zao, kutokana na agizo la Inspekta Mkuu wa Polisi Hillary Mutyambai.

Mutyambai alisema viongozi wote walio kwenye uchunguzi ni lazima wasalimishe silaha zao, wakiwamo seneta wa Nandi Samson Cherargei, wabunge Moses Kuria, Aisha Jumwa na Babu Owino.