• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Karibuni Mombasa lakini…

Karibuni Mombasa lakini…

CHARLES WASONGA NA BENSON MATHEKA

VIONGOZI wanaounga mkono mchakato wa maridhiano (BBI) wamewakaribisha wenzao wa mrengo wa Tangatanga katika mkutano wao wa kuvumisha mapendekezo ya jopokazi hilo mjini Mombasa lakini kwa masharti kadhaa.

Wabunge Junet Mohammed (Suna Mashariki), Kanini Kega (Kieni), Fatuma Gedi (Mbunge Mwakilishi, Wajir) na Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja walitaka wenzao ambao ni wandani wa Naibu Rais William Ruto kufika katika mkutano huo kwa nia njema.

“Tunakaribisha uamuzi wao wa kuungana nasi katika mchakato huu wa kuunganisha Wakenya. Hata hivyo, wanafaa kuwa na nia njema bila kutoa masharti yoyote,” akasema Bw Mohammed ambaye ni kiranja wa wachache katika bunge la kitaifa.

Mnamo Jumanne, wabunge wanaomuunga Dkt Ruto walitangaza kwamba, watakuwa wakihudhuria mikutano ya kujadili ripoti hiyo ambayo walikuwa wamepinga wakisema ilikuwa ya kupoteza wakati na pesa.

Wakihutubia wanahabari katika mkahawa wa Serena, Nairobi, wabunge hao walisema kwamba, wameamua wawe wakihudhuria mikutano hiyo na kushiriki mijadala ya kuboresha ripoti ya BBI ili isitekwe na wanasiasa ambao ajenda yao kuu ni kutafuta mbinu za kugawana mamlaka.

Waliapa kutumia mikutano hiyo na kuhakikisha BBI itashughulikia ukosefu wa ajira na utawala wa sheria miongoni mwa masuala mengine.

Na Jana, Bw Mohamed alisema wote wamekaribishwa kushiriki mikutano ya kujadili BBI lakini akaonya kuwa hawataruhusu wanasiasa hao kupotosha Wakenya kwamba mchakato huo unahusu siasa za 2022.

“BBI ni ya kuunganisha Wakenya na hata katika mikutano miwili iliyotangulia Kisii na Kakamega, siasa za 2022 hazikujadiliwa,” alisema.

Naye Bw Kega alisema kwamba, wanawakaribisha wabunge hao kwenye mikutano ya BBI lakini akawaonya dhidi ya kutomheshimu Rais Uhuru Kenyatta ambaye aliasisi mchakato huo akiwa pamoja na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Wakati huo huo, Seneta wa Kaunti ya Kakamega Cleophas Malala mnamo Jamatano alitoa sharti jingine kwa wanachama wa Tangatanga. Alisema waandaliza wa mkutano wa Mombasa hawatazingatia itifaki na kwamba, kiongozi wa ODM Raila Odinga ndiye atahutubu wa mwisho katika mkutano huo hata kama Dkt Ruto atakuwepo.

“Rais Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga ndio vinara wawili, na wa kipekee, wa mchakato wa BBI. Kwa hivyo, endapo Rais hatahudhuria mkutano wa Mombasa, Raila ndiye ataongea wa mwisho hata kama Ruto atakuwepo,” akasema Jumanne usiku katika kipindi cha ,”Sidebar” kwenye runinga ya NTV.

Akaongeza: “Tunawaalika wanachama wa Tangatanga katika mikutano yetu ya BBI lakini wajue kuwa kinara wao sharti atii itifaki yetu sio ile ya serikali. Ile yao inatumika tu katika sherehe za kitaifa.”

Bw Malala, ambaye ni naibu kiongozi wa wachache katika seneti, alisisitiza kuwa itifaki ya serikali ambapo Bw Odinga huongea kabla ya Dkt Ruto haitatumika katika mikutano ya BBI “kwa sababu handisheki ilikuwa kati ya watu wawili pekee.”

Washirika wa Dkt Ruto walisusia mikutano ya awali mijini Kisii na Kakamega wakisema haikufaa kwa sababu hakuna anayepinga ripoti iliyozinduliwa Novemba 27 katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi.

Naye akiongea katika kaunti ya Vihiga wiki jana, Dkt Ruto aliikosoa mikutano hiyo akisema ilikuwa ni kufuja tu pesa za umma.

Na juhudi za wandani wake kutoka uliokuwa mkoa wa magharibi za kuandaa mkutano wao sambamba mjini Mumias zilizimwa na maafisa wa polisi.

Lakini Jumanne, washirika wake, wakiongozwa na seneta wa Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen walidai kuna njama fiche za kuandaa ripoti tofauti na iliyozinduliwa Bomas na kukubalika na Wakenya wote.

You can share this post!

AKILIMALI: Waungama, maembe yana pato la uhakika

BONGO LA BIASHARA: Anajikimu na wenzake 3 kupitia jiko hili...

adminleo