• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 11:13 AM
‘Inahitajika dharura kuokoa elimu ya mtoto wa kiume Lamu’

‘Inahitajika dharura kuokoa elimu ya mtoto wa kiume Lamu’

Na KALUME KAZUNGU

OFISI ya Idara ya Elimu, Kaunti ya Lamu imeelezea hofu yake katika kile imetaja ni kusahaulika kwa elimu ya mtoto wa kiume eneo hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa Elimu, Kaunti ya Lamu, Joshua Kaaga, anasema kumekuwa na kampeni nyingi hasa za kielimu zinazoelekezewa mtoto wa kike Lamu ilhali wale wa kiume wakikosa kampeni hizo.

Katika mahojiano na ‘Taifa Leo’ ofisini mwake, Bw Kaaga alitaja kuboreshwa kwa miundomsingi zaidi hasa kwa shule za wasichana Lamu ilhali wale wa kiume wakiachwa hivyo.

Kaunti ya Lamu ina shule mbili pekee za bweni kwa wavulana – ile ya Lamu na ile ya Mpeketoni.

Afisa huyo anawataka wahisani kujitolea kikamilifu ili kuboresha miundomsingi kwa shule hasa za wavulana eneo hilo ili elimu iende sambamba kwa jinsia zote.

Hofu yake ni kwamba endapo elimu ya mtoto mvulana itaendelea kusahaulika, huenda ikachangia utovu wa usalama miongoni mwa jamii eneo hilo.

“Nimekuwa nikichunguza na kubaini kuwa kampeni nyingi za kielimu hapa Lamu na poia nchini kwa jumla zinaelekezewa mtoto wa kike ilhali wale wa kiume wakisahaulika. Suala hili likiwa halitarekebishwa huenda likachangia utovu wa usalama miongoni mwa jamii zetu. Ni vyema kampeni za kielimu zifanywe kwa wanafunzi wa jinsia zote ili kuwe na usawa katika maendeleo ya kielimu Lamu na nchini kwa jumla,” akasema Bw Kaaga.

Wakati huo huo, Ofisi ya Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia, imetoa onyo kali kwa wazazi watakaozembea katika kuwapeleka watoto wao shule.

Bw Macharia anasema ameelekeza idara ya polisi kuwakamata na kuwashtaki wazazi na hata wanafunzi watakaopatikana wakirandaranda ovyo mitaani licha ya kutimiza umri wa kwenda shule.

“Sitakubali mtoto yeyote kurandaranda mitaani ovyo wakati ana umri wa kwenda shule. Polisi wakikupata wewe mtoto utakamatwa pamoja na mzazi wako mshtakiwe. Lazima elimu izingatiwe na iheshimiwe,” akasema Bw Macharia.

You can share this post!

Hatima ya Waititu kuamuliwa wiki ijayo – Lusaka

Pesa zinazomwagwa wakati wa kampeni zaiponza Kenya

adminleo