Kimataifa

Watu 3 wafariki wakizima moto nchini Australia

January 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na AFP

SIDNEY, Australia

WAHUDUMU watatu wa ndege ya shirika moja la huduma za zimamoto wamefariki Alhamisi wakipambanaa na moto Kusini mwa Sydney, Australia ndege yao ilipoanguka, maafisa wa Australia wamesema.

Kamishna wa Shirika la New South Wales Rural Fire Service Shane Fitzsimmons amesema mawasiliano kati ya maafisa wa serikali na ndege hiyo, aina ya C-130 Hercules, iliyokuwa ikihudumu eneo la Monaro, yalikatizwa Alhamisi asubuhi.

Fitzsimmons amesema watu wote watatu waliofariki katika ajali hiyo walikuwa raia wa Amerika, moja kati ya mataifa kadhaa ambayo yametuma wataalamu wa kupamba na mikasa ya moto nchini Australia.

“Tunaungana na wale wote wanaathirika kufuatia vifo vya wahudumu watatu ambao wametumia miaka yao mingi wakifanya kazi ya kupambana na moto,” akasema.

Kisa hicho kinafikisha 32 idadi ya watu ambao wamefariki kutokana na mikasa ya moto nchini Australia tangu Septemba 2019.

Chanzo cha ajali hiyo hakikujulikana mara moja, lakini Fitzsimmons amesema awali kwamba upepo mkubwa unaovuma umefanya shughuli ya kuzima moto “kuwa ngumu” zaidi.

Kufuatia ajali hiyo, kampuni ya ndege ya Coulson Aviation inayomiliki ndege iliyohusika katika ajali imesitisha shughuli za ndege zake zingine ambazo zilikuwa zikitumika kupambana na moto katika majimbo ya New South Wales na Victoria.