• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Rais Kenyatta akosa kusoma sehemu ya hotuba yake ‘kudumisha amani’

Rais Kenyatta akosa kusoma sehemu ya hotuba yake ‘kudumisha amani’

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amekwepa kusoma maneno makali katika hotuba yake, iliyoandikwa, aliyowasilisha katika majengo ya Mahakama ya Juu, Nairobi.

Akiongea katika sherehe ya uzinduzi wa ripoti kuhusu Hali ya Idara ya Mahakama na Usimamizi wa Haki ya kati ya 2018 na 2019, Rais Kenyatta amesita mara kadhaa Alhamisi, akisema kuwa amekwepa kusoma sehemu ya hotuba yake ili “kudumisha amani.”

Tofauti na hali ilivyo katika shughuli za awali ambapo Rais alishambulia Idara ya Mahakama hadharani, Alhamisi aliamua kukumbatia ‘moyo wa urafiki’, ulioanzishwa na Jaji Maraga aliyehutubu kabla yake.

Kinyume na kawaida yake, Bw Maraga alikuwa mnyenyekevu katika hotuba yake huku akitoa wito kwa Rais kuipiga jeki idara ya mahakama kwa kuongeza bajeti yake.

“Tunaomba utusaidie kwa kuamuru Hazina ya Kitaifa ituongezee mgao wa fedha katika bajeti ili tuweze kufadhili miradi na mipango yetu kote nchini,” Maraga akaomba kwa upole.

Mwaka 2019 Jaji Mkuu aliisuta Serikali Kuu akidai baadhi ya maafisa wake wanahujumu Idara ya Mahakama kwa kupunguza mgao wake wa fedha kwenye bajeti “bila sababu”.

Huku akilalamikia kunyanyaswa na kutopewa heshima inavyostahiki, Bw Maraga alitisha kukwepa hafla za kitaifa.

Na kweli Bw Maraga hakuhudhuria Sherehe za Kitaifa za Jamhuri zilizofanyika Desemba 12, 2019, katika Uwanja wa Nyayo, Nairobi.

Kiti alichotengewa, chenye jina lake, kilisalia wazi hadi sherehe hizo zilipomalizika kwa sababu hakufika.

Alhamisi, Jaji Maraga amejitetea kutokana na matamshi aliyotoa wakati huo akisema, alieleweka vibaya na hakumshambulia Rais.

“Wewe ni Mkuu wa Serikali na Kiongozi wa Taifa. Wewe ni ishara ya Umoja wa Kitaifa na ninatambua hilo,” amesema Bw Maraga.

Rais Kenyatta amesema maombi ya Jaji Maraga yana mashiko, lakini akaongeza kuwa idara ya mahakama inastahili kutumia rasilimali zilizopo kwa “uangalifu”.

“Tutajikaza kuwasaidia mpate pesa za kutosha lakini ninyi pia mwafaa kukomesha ubadhirifu. Badala ya kufanya mikutano yenu Mombasa mwafaa kutumia hoteli za hapa Nairobi ili kupunguza gharama,” akasema.

You can share this post!

Wafanyakazi watano wa kaunti ya Kiambu wakanusha shtaka la...

Watu 3 wafariki wakizima moto nchini Australia

adminleo