• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:07 PM
Tobiko asema jamii ya Maasai inaunga mkono BBI

Tobiko asema jamii ya Maasai inaunga mkono BBI

Na LAWRENCE ONGARO

JAMII ya Maasai imehimizwa kuunga serikali mkono kwenye mpango wa maridhiano wa BBI.

Waziri wa Mazingira na Maliasili Bw Keriako Tobiko, aliongoza viongozi kadha wa Maasai na wasomi kwenye afisi yake leo Ijumaa ili kuunga mkono kwa dhati mpango wa maridhiano wa BBI.

“Leo tumejumuika hapa kuunga mkono mpango wa serikali wa kueneza ushirikiano mwema kupitia BBI. Sisi kama jamii ya Maasai tuko ndani ya BBI na hakuna kurudi nyuma,” alisema Bw Tobiko.

Alisema viongozi wa jamii hiyo watafanya juhudi kuona ya kwamba jamii ya Maasai inakuwa mstari wa mbele kuipigia debe BBI kwa lengo la kunufaika na rasilimali zilizoko katika eneo lao.

Viongozi hao walijadiliana mengi kuhusu jinsi jamii yao ina rasilimali tosha za kuwasukuma mbele katika maisha yao ya baadaye.

“Iwapo BBI itapitishwa na Wakenya, bila shaka tuko katika nafasi nzuri ya kufaidika kutokana na mazingira tunayoishi kama jamii. Kwa hivyo tutafanya juhudi kuona ya kwamba jamii yetu inaelezewa umuhimu wa BBI na manufaa yake katika siku za usoni,” alisema Bw Tobiko.

Walijadiliana mengi kuhusu jinsi serikali ina mipango kabambe ya kuzindua miradi tofauti katika eneo lao na kwa hivyo huu sio wakati wa kukaidi maswala ya serikali.

Wakati wa mkutano huo viongozi hao kwa kauli moja walikubaliana ya kwamba hivi karibuni wataanza kuzunguka katika maeneo tofauti ili kuhamasisha Wamaasai umuhimu wa BBI na manufaa yake.

“Tutakuwa katika mstari wa mbele kuona ya kwamba tunahamasisha jamii yetu na kupata maoni yao kuhusu BBI na watatueleza pia matakwa yao ili yaweze kujumuishwa katika ripoti hiyo,” alisema Bw Tobiko.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria hafla hiyo kwenye afisi ya waziri huyo ni, katibu wa idara ya nchi na ugatuzi, Bw Charles Sunkuli. Wengine ni Dkt Richard Ole Lesiyampe, Bw David Kedienye, Bw Simon Ole Kirigoti, Bw Joseph Musuni, Bw George Ole Meshuko, Bw Jonathan Pasha (MUA), Bw Alfred Ole Keriolale, Bw Mark Melek Leleruk, na Bw Alex Lemarkoko.

You can share this post!

China yatenga watu 30 milioni miji 10 kutokana na virusi

‘Asilimia kubwa ya mishahara ya wafanyakazi mijini...

adminleo