Wakenya walio China waomba serikali iwafikirie
Na ELIZABETH MERAB
WAKENYA wanaoishi China wameeleza wasiwasi wao kwamba serikali haijafanya juhudi za kutosha kuwalinda dhidi ya virusi hatari vya homa ya CoV (Coronavirus) inayoendelea kusababisha vifo nchini humo.
Zaidi ya watu milioni 48 mnamo Jumamosi waliwekwa chini ya uangalizi mkali katika miji 15 katika mkoa wa Hubei, kama njia ya kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo.
Wanafunzi kutoka Kenya ambao wamekuwa wakiishii miji mbalimbali ya China waliozungumza na Taifa Leo, walieleza wasiwasi wao kuhusu kimya cha serikali yao.
“Sijasikia lolote kutoka kwa ubalozi wetu. Walituuliza tu kupitia viongozi wetu jinsi hali ilivyo nyanjani tangu kuzuka kwa virusi hivyo,” akasema mwanafunzi mmoja kutoka Beijing.
Kwa mujibu wa wanafunzi hao, ubalozi wa Kenya nchini China ulituma mwakilishi aliyetambulika tu kama Dkt Robert ili kufikia kundi la wanafunzi wanaoishi Beijing, wakiomba nambari za simu za Wakenya wanaoishi jiji la Wuhan.
Jiji hilo limekuwa kitovu cha virusi hivyo na ni kati ya miji ambayo wakazi wake wamezuiwa kusafiri hadi miji mingine.
“Habari za mchana, kutokana na mkurupuko wa virusi vya CoV jijini Wuhan, ubalozi wa Kenya unaomba nambari za mawasiliano za Wakenya wote jijini Wuhan,” ukasema ujumbe wa Dkt Robert kwa kundi la wanafunzi jijini Beijing.
Ingawa wanafunzi katika miji ya Beijing, Wuhan na Xian walisema kwamba kwa sasa wako salama, wasiwasi wao ni kimya cha maafisa wanaohudumu katika ubalozi wa Kenya ambao hawaonekani kushughulishwa na mkurupuko huo.
“Kwa sasa tuko sawa japo hatujaruhusiwa kutoka eneo moja hadi jingine ila tu ukienda kununua vyakula. Hata katika hali hiyo, tunalazimika kufunika nyuso zetu,” akasema mwanafunzi Mkenya anayesomea katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Kiteknolojia cha Guazhoung.
Idadi ya wanafunzi Wakenya wanaoishi katika mji wa Wuhan ambao umeathirika zaidi na virusi vya COV ni 100.
Ingawa ‘Taifa Leo’ haitafichua majina ya wanafunzi hao kwa sababu wengi wao wako chini ya ufadhili wa kimasomo kutoka kwa serikali ya China, wengi wao walieleza kwamba hawajakosa bidhaa muhimu ila tu wamezuiwa kuondoka sehemu moja hadi nyingine.
“Wengi wetu tumelazimika kusalia majumbani kwa hofu ya kuambukizwa virusi hivyo. Kuna hofu kwamba huenda tukakosa vyakula siku chache zijazo kwa sababu hoteli nyingi na vituo vya kuuza vyakula sasa vinaendelea kufungwa. Kupitia kwa uungwaji mkono wa serikali yetu na maombi, tuna matumaini kwamba tutasalia salama,” akasema mwanafunzi jijini Wuhan.
Haya yanatokea huku China ikianza sherehe za kukaribisha mwaka wake mpya huku onyo likitolewa ili mikakati ya kutosha iwekwe kuzuia virusi hivyo kusambaa na kuwaua watu zaidi.
Ikizingatiwa kwamba virusi hivyo husambaa kutoka kwa binadamu hadi mwingine, serikali ya China imeamrisha raia wote nchini China wazuiwe kusafiri kutoka eneo moja hadi jingine.
Baadhi ya mataifa kama Marekani, Ufaransa na Urusi nayo yameanza kuwahamisha raia wao wanaoishi jijini Wuhan licha ya amri ya kutosafiri iliyotolewa na China.