Wazito wageuzwa wepesi na Gor
Na CHRIS ADUNGO
FOWADI Jacques Tuyisenge aliwafungia Gor Mahia bao muhimu lililowachochea kuwabamiza limbukeni Wazito FC 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya KPL iliyowakutanisha jana ugani Kenyatta, Machakos.
Ingawa ushindi huo wa Gor Mahia uliwadumisha katika nafasi ya pili jedwalini kwa alama 22, wafalme hao mara 16 wa taji la KPL walipunguza pengo la alama kati yao na viongozi Mathare United hadi pointi moja.
Nafuu zaidi kwa kocha Dylan Kerr ni kwamba Mathare United ambao watavaana na Posta Rangers wikendi hii wametandaza jumla ya michuano 10, miwili zaidi kuliko Gor Mahia. Tuyisenge alitoka benchi katika kipindi cha pili na kuwapa Gor Mahia ushindi muhimu kunako dakika ya 74 baada ya kukamilisha kwa kichwa mkwaju wa ikabu.
Gor Mahia walitumia mchuano huo kama jukwaa mwafaka zaidi la kujinoa kwa mechi ya marudiano dhidi ya SuperSport ya Afrika Kusini kwenye Kombe la Mashirikisho barani Afrika (CAF Confederations Cup).
Ushindi wa Gor Mahia kwa sasa unawasaza Wazito katika nafasi ya 12 jedwalini kwa alama 11. Baada ya kuvaana na Chemelil Sugar mwishoni mwa wiki hii, Wazito wamepangiwa kuonana na Mathare, Tusker na Sofapaka kwa usanjari huo.
Kwingineko, kocha Ken Odhiambo wa Bandari aliwatoa wasiwasi mashabiki wa timu hiyo hapo jana kuhusu hali ya mwanasoka wa timu ya taifa ya Harambee Stars U-23, Nicholas Meja kwa kusisitiza kwamba amepona jeraha.
Odhiambo alisema kuwa Meja anaendelea na mazoezi yuko katika kikosi kinachotarajiwa kuondoka kuelekea Bungoma kwa mechi dhidi ya Nzoia Sugar itakayopepetwa uwanjani Sudi hapo Jumapili.
Aidha, alifichua kuwa kikosi chake kitakosa huduma za straika mkongwe Shaaban Kenga ambaye alijitonesha kisigino wakati wa mechi iliyopita dhidi ya Ulinzi Stars ugani Mbaraki Sports Club.
Kwa wakati huu, Bandari inashikilia nafasi ya tano ikiwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi tisa, kushinda nne, kutoka sare mara tatu na kupoteza mechi mbili. Mastraika wake wamefunga mabao tisa na kikosi kimefungwa mabao manne.
Wakati uo huo, kocha Sammy ‘Pamzo’ Omollo wa Posta Rangers amekiri kwamba kurejea kwa nyota Dennis Mukaisi ni afueni kubwa itakayowapiga jeki vijana wake watakaovaana na Mathare United mwishoni mwa wiki hii.
Mukaisi anatazamia kupangwa katika kikosi cha kwanza baada ya jeraha kumweka mkekani kwa zaidi ya miezi mitatu iliyopita. Mvamizi huyo wa zamani wa Tusker na Leopards aliwajibishwa kwa mara ya kwanza msimu huu katika mchuano wa wikendi jana uliowashuhudia Rangers wakibamizwa 1-0 na Zoo Kericho.
Rangers kwa sasa wanashikilia nafasi ya saba jedwalini kwa alama 14.