• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 4:50 PM
Mama adaiwa kuiba bunduki ya mlinzi wa makao ya Naibu wa Rais

Mama adaiwa kuiba bunduki ya mlinzi wa makao ya Naibu wa Rais

Na BRIAN OCHARO

POLISI anayelinda makazi ya Naibu Rais William Ruto jijini Mombasa alipoteza bunduki yake katika hali ya kutatanisha, alipompeleka mwanamke katika makazi hayo, Mahakama ya Mombasa ilielezwa Jumatatu.

Mahakama hiyo iliambiwa kuwa, afisa Francis Kariuki kutoka kituo cha Central jijini humo alipoteza silaha hiyo iliyokuwa na risasi, usiku wa Desemba 18, 2019.

Ilidaiwa mahakamani kuwa Bw Kariuki alikutana na mwanamke huyo aliyejitambulisha tu kama Bi Stella, karibu na jumba la Housing Finance kwenye barabara ya Moi katikati mwa jiji la Mombasa mwendo wa saba usiku.

Walizungumza na kukubaliana kuondoka pamoja hadi nyumbani kwa afisa huyo, iliyo katika makazi ya Naibu Rais baada ya kuafikiana kuhusu bei ya huduma za ngono ambazo Bi Stella angetoa.

Kulipopambazuka, afisa huyo aligutuka kukosa bunduki na simu yake, naye mwanamke huyo hakuwa chumbani.

Mnamo Januari 14, polisi walifanikiwa kumkamata Joshua Owiti Oliech katika eneo la Kisauni akiwa na simu iliyoibwa kutoka kwa afisa huyo.

Hiyo Jumatatu, Bw Oliech alishtakiwa pamoja na mwanamke kwa jina Elias Wakesho Kazungu kwa tuhuma za kuiba bastola iliyokuwa na risasi 15.

Upande wa mashtaka ulisema washukiwa waliiba bastola hiyo , risasi na simu ya thamani ya Sh1,200 kutoka katika makazi hayo ya Naibu Rais yaliyo eneobunge la Mvita.

Upande wa mashtaka ulisema washukiwa walitekeleza makosa hayo pamoja na wengine ambao bado wanasakwa.

Simu hiyo aina ya Itel ilikuwa ikimilikiwa na Bw Kariuki. Pia washukiwa walishtakiwa kwa kuiba bastola na risasi ambazo ni mali ya Kikosi cha Huduma za Polisi (NPS).

Bw Oliech pia alishtakiwa kwa kosa lingine la kupatikana na mali iliyoibwa.

Alishtakiwa kwamba mnamo Januari 14 katika eneo la Kisauni, alipokea simu hiyo akifahamu kwamba ilikuwa imeibwa.

You can share this post!

TAHARIRI: Kulipa watu wazae ni mzaha usiofaa

‘Tangatanga’ warai Rais ataje chaguo lake kura...

adminleo