Hali ya usalama yazorota kijijini Kwambira, Limuru
Na LAWRENCE ONGARO
WAKAZI wa kijiji cha Kwambira mjini Limuru wanataka usalama uimarishwe haraka iwezekanavyo.
Wakazi hao wanasema kwa miezi michache wamekuwa wakishambuliwa na wahuni ambao ni vijana wadogo.
Mwenyekiti wa wenye karakana za eneo hilo Bw Peter Ndung’u alisema wananchi hawataki kupiga ripoti kwa polisi wakiogopa kutambuliwa na wahuni hao.
“Tumegundua ya kwamba wengi wao hujificha maeneo haya ya karakana zetu nyakati za usiku na jioni huku wakivizia wapitanjia kwa kuwadunga kwa kisu na kuwapora,” alisema Bw Ndung’u.
Alisema kila mwezi hakukosi visa viwili vya aina hiyo ambavyo hushuhudiwa lakini polisi hawafahamishwi.
Msusi Bi Esther Mbugua anayemiliki duka lake mjini Limuru anasema ya kwamba duka lake limevamiwa zaidi ya mara saba na mali ya thamani kubwa kuibwa,
“Mimi karibu mara kadha wahuni wamevunja duka langu na kuiba vifaa vinavyoweza kugharimu laki tano na zaidi,” alisema Bi Mbugua.
Wakazi hao walisema wahuni wanaohusishwa na wizi huo ni wa umri wa kati ya miaka 17-25 na wengi wao hujihami kwa visu na cha kushangaza ni kwamba wao humtaja mtu kwa jina kabla ya kumpora.
Naibu kamishna wa eneo la Limuru Bw Charles Mukele alisema tayari wamepata habari kamili kuhusu matukio hayo na wako macho kukabiliana nayo.
“Sisi kama walinda usalama tumeweka mikakati kabambe ya kukabiliana na wahuni hao ambapo tunawahakikishia wananchi wa Limuru ya kwamba wataona mabadiliko ya kiusalama hivi karibuni,” alisema Bw Mukele.
Aliwahimiza wananchi kuwa mstari wa mbele kushirikiana na polisi ili kuwanasa wahuni hao ambao wanahangaisha wakazi wa Limuru.
“Iwapo mtu ana majina halisi ya wahuni hao tafadhali niletee kwa afisi yangu ili tuweze kuchukua hatua inayostahili. Tutaiweka kama siri bila kutaja aliyetuarifu majina hayo,” alisema afisa huyo.