Polisi bandia akamatwa baada ya kumtia mbaroni mwanafunzi
Na BENSON MATHEKA
POLISI jijini Nairobi wanafanya uchunguzi kubaini jinsi mwanamume alivyoingia katika chuo cha kitaifa cha kiufundi cha Kabete na kumkamata mwanafunzi mmoja akijifanya afisa wa polisi.
Inadaiwa kwamba Bw Daniel Ochieng, 23 alienda katika chuo hicho Jumanne mchana na kujitambulisha kama afisa wa polisi kutoka kituo cha Central aliyekuwa kazini.
Kulingana taarifa ya idara ya kupeleleza uhalifu nchini (DCI), Bw Ochieng alidai kwamba alikuwa ametumwa kuchunguza vitendo vya uhalifu katika chuo hicho.
“Alienda katika chuo hicho na kujitambulisha kama afisa wa polisi aliyetumwa kutoka kituo cha polisi cha Central kuchunguza vitendo vya uhalifu,” DCI ilisema kwenye taarifa katika anwani yake ya Twitter.
Taarifa ilisema kwamba alimkamata mwanafunzi mmoja akimlaumu kwa kuhusika na ulanguzi wa dawa za kulevya.
“Alitisha kumchukulia mwanafunzi huyo hatua kali na katika harakati hizo akapatiwa hongo ya Sh30,000,” DCI ilieleza.
Hata hivyo, mwanafunzi huyo alipiga ripoti kwa maafisa wa usalama ambao walimsaka na kumkamata mshukiwa.
Polisi walisema walipomkamata walimpata na Sh30,000, misokoto ya bangi na bastola bandia. Baada ya uchunguzi mshukiwa anaweza kushtakiwa kwa kujifanya afisa wa polisi, kupatikana na dawa za kulevya na kupatikana na silaha bandia.
Wakazi wa eneo hilo walisema visa vya uhalifu vimeongezeka karibu na chuo hicho na wakataka polisi kuongeza doria.