Nzige ni chakula kizuri, wataalamu washauri
Na WINNIE ATIENO
WATAALAMU wa hali ya hewa na tabianchi na wenzao wa lishe bora wamewasihi Wakenya wavune nzige waliovamia zaidi ya kaunti 10 nchini na kusababisha uharibifu mkubwa wa mimea.
Aidha wanasema nzige hao wanafaa kuvunwa, kukaushwa na baadaye kutumiwa kama lishe kwa binadamu, samaki na hata kuku huku wakisisitiza kuwa wadudu hao wanaweza kutumiwa kudhibiti baa la njaa.
“Kuna baadhi ya jamii ambazo hula nzige ama wakiwa wabichi au hata wakiwa wamechomwa na kupikwa. Kimsingi, nzige ni chakula duniani na kumekuwa na mjadala mkuu endapo wadudu wanaweza kuliwa kama chakula hasa wakati kuna baa la njaa ulimwenguni,” akasema Dkt Richard Muita.
Akiongea kwenye kongamano la kudadisi hali ya hewa na tabianchi barani Afrika, Dkt Muita alisema nzige hao wana protini zaidi kuliko hata nyama ya ng’ombe.
“Nzige wanalika na wana protini; nakumbuka ujana wangu nilikuwa nawala sana. Tusiangalie ubaya wa uvamizi wa nzige hawa nchini, badala yake tudadisi umuhimu wa wadudu hawa ambao wanaweza kutumika pia kama lishe kwa kuku na samaki,” alisema.
Dkt Muita ambaye anafanya kazi katika idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini, alisema wadudu hao wanaweza kuvunwa, kukaushwa juani na baadaye kuliwa.
“Hapo tutakuwa tumeweza kudhibiti uvamizi huu, badala ya kunyunyizia dawa,” alisema.
Mtaalamu wa lishe bora, Bi Martina Adega alisema ulaji wa wadudu hao unaweza kupunguza maradhi ya moyo ikizingatiwa nzige wana protini.
Hata hivyo, changamoto kuu ambayo Kenya inakodolea macho ni ukosefu wa mashine za kutengeneza vyakula vya mifugo.
“Hata kama tunadhamiria kuvuna nzige hao, watakaushwa wapi? Je, tunamashini ya kuzisaga ili tutengeneza vyakula vya wanyama kama paka, mbwa, kuku, samaki?” aliuliza Bi Adega.
Alisema protini inayopatikana katika nzige ni ya ubora wa hali ya juu.
Naye mfanyakazi wa Wizara ya kilimo, Bw James Wanjohi, alisema wadudu hao walivamia Kenya Disemba 28, 2019, na kufikia sasa serikali imejizatiti kukabiliana na wadudu hao ili wasiendelee kuharibu mimea.
Bw Wanjohi alisema maafisa wengi wanafaa kupewa mafunzo ya kukabiliana na wadudu hao.