JAMVI: Kauli za Rais zaonyesha huenda asing’atuke madarakani 2022

Na WANDERI KAMAU

KAULI mbalimbali za Rais Uhuru Kenyatta kuhusu mustakabali wake wa kisiasa zimeonyesha kuwa huenda asing’atuke mamlakani baada ya muda wake kuisha katika mwaka wa 2022.

Pamekuwapo wasiwasi kuhusu ikiwa Rais Kenyatta ataondoka uongozini huku ikikosa kudhihirika hadi sasa ikiwa ataondoka kama alivyoahidi au la.

Hali hiyo ilidhihirika Jumapili iliyopita, aliposema kwamba “ataelekea kwa familia yake” baada ya kuacha kazi muda wake utakapoisha.

Hata hivyo, kauli hiyo ni tofauti na semi zake za awali, ambapo amenukuliwa akisema kwamba akipewa nafasi ya kuhudumu serikalini bila shaka atachukua.

Alitoa kauli hiyo mnamo Novemba iliyopita kwenye mkutano uliofanyika katika eneo la Sagana, uliowashirikisha viongozi mbalimbali kutoka eneo la Mlima Kenya.

“Sitajali kuhudumu serikalini ikiwa wananchi watanirai kufanya hivyo,” alisema Rais.

Kauli hii inawiana na nyingine aliyotoa mnamo 2018 katika Kaunti ya Nyeri, aliposema kuwa ni “Mungu tu ajuaye atakayeitawala Kenya baada ya 2022.”

Semi zake pia zimekuwa zikikaririwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wafanyakazi (COTU), ambaye amekuwa akisisitiza kuwa Rais Kenyatta “ni mchanga sana kuondoka uongozini.”

“Mnataka Rais (Uhuru) aende wapi? Angali kijana!” akaeleza Bw Atwoli.

Kutokana na semi hizo, wachanganuzi wanasema kuwa hali ilivyo, ni dhahiri kuwa Rais hayuko tayari kuondoka uongozini, lakini hataki kuwadhihirishia wananchi mapema.

Kulingana na wakili Ndegwa Mwangi, ambaye ni mchanganuzi wa siasa, kuna sababu kadhaa ambazo zinaashiria huenda Rais Kenyatta asing’atuke uongozini baada ya 2022.

Mojawapo ya sababu hizo ni ukosefu wa mrithi wa kisiasa kutoka Mlima Kenya, akisema kuwa hadi sasa, hakuna kiongozi yeyote ambaye anaonekana kuliunganisha eneo hilo kisiasa kama ambavyo amefanya Bw Uhuru tangu Rais Mstaafu Mwai Kibaki alipong’atuka uongozini mnamo 2013.

“Ingawa kuna viongozi kadhaa ambao wamependekezwa kujaza nafasi atakayoacha Rais Kenyatta ikiwa atang’atuka uongozini, wengi hawana ushawishi alio nao. Hivyo, hilo linaifanya vigumu kwake kuliacha eneo hilo,” asema Bw Mwangi.

Baadhi ya viongozi ambao wametajwa kuwa warithi wa Rais Kenyatta kisiasa katika eneo hilo ni magavana Francis Kimemia (Nyandarua), Anne Waiguru (Kirinyaga), Mwangi wa Iria (Murang’a), aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri kati ya wengine.

Hata hivyo, wachanganuzi wanasema kuwa kati ya wale waliopendekezwa kuchukua nafasi hiyo, hakuna anayekubalika kikamilifu na jamii za Agikuyu, Aembu na Ameru (GEMA).

“Kiongozi ambaye atamrithi Rais Kenyatta lazima awe na ushawishi wa kutosha kuziunganisha jamii hizo zote. Ilivyo sasa, ni Bw Kenyatta pekee anayeonekana kuwa na ushawishi wa kiwango hicho. Hiyo bila shaka ni mojawapo ya sababu kuu ambapo huenda asing’atuke,” asema Bw Mwangi.

Wachanganuzi pia wanataja mvutano wa kisiasa kati ya jamii hizo kuhusu uongozi kama chanzo kingine ambacho huenda kikachangia Rais Kenyatta kutong’atuka.

Jamii za Aembu, Ameru na Mbeere zimetishia kutomuunga mkono kiongozi mwingine wa kisiasa kutoka jamii ya Agikuyu, zikidai kuwa jamii hiyo inapaswa “kuwarudishia mkono” kwa kuwaunga viongozi wake tangu uhuru.

Harakati hizo zimekuwa zikiendeshwa kichinichini na Gavana Kiraitu Murungi (Meru), akitishia kuwaongoza viongozi wa eneo la Mlima Kenya Mashariki kujiondoa katika Chama cha Jubilee (JP) ikiwa mrithi wa Rais Kenyatta hatatoka katika eneo hilo.

“Nitabuni chama huru cha eneo hili kama njia moja ya kulalamikia eneo la Mlima Kenya Mashariki kutopewa nafasi ya kuuongoza ukanda wa Mlima Kenya kisiasa. Lazima mrithi wa Rais Kenyatta asitoke katika eneo la Kati,” akasema Bw Murungi.

Tayari, kauli za Rais Kenyatta zimeibua hali ya wasiwasi miongoni mwa viongozi wa kisiasa katika eneo hilo, baadhi wakianza harakati za kusajili vyama mbadala, kama matayarisho ya mwelekeo wa kisiasa mnamo 2022.

Miongoni mwa vyama ambavyo tayari vimesajiliwa ni Transformation National Alliance (TNAP) kinachohusishwa na mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, The Service Party (TSP) kinachohusishwa na Bw Kiunjuri, Civic Renewal Party (CRP) kinachohusishwa na Bw Wa Iria kati ya vingine.

Wachanganuzi wanasema kuwa lengo kuu la viongozi hao ni kujitayarisha kwa mwelekeo wowote wa kisiasa ambao nchi itajipata ikiwa Rais atang’atuka uongozini au la.

“Bila shaka, viongozi hao wanafahamu kuwa huenda Rais Kenyatta asing’atuke uongozini lakini watahitaji kujiendeleza kisiasa. Hiyo ndiyo sababu kuu ambapo baadhi yao wako mbioni kujijenga kabla ya uchaguzi huo kufika,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Wachanganuzi pia wanasema kuwa huenda kauli ya Rais Kenyattta imechangiwa na mabwanyenye, hasa katika eneo hilo, wanaotajwa kuhofia uongozi wa Naibu Rais William Ruto kama rais.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wanashikilia kuwa Rais Kenyatta hana mpango wowote wa kuendelea kukwamilia mamlakani, wakisema kuwa wakosoaji ndio wanafasiri kauli zake visivyo.

“Rais Kenyatta ni kiongozi anayeheshimu na kuzingatia mfumo wa demokrasia. Wanaosema ana mipango ya kuendelea kuwepo serikalini ni watu wenye nia ya kumharibia jina,” asema mbunge wa Kieni, Kanini Keega.

Habari zinazohusiana na hii

Ahadi juu ya ahadi

Ruto ararua BBI

MANAHODHA WA DOMO DOMO