HabariSiasa

JAMVI: Ukaidi wa Ruto kwa Rais wafika kilele, nani atashinda?

February 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na VALENTINE OBARA

UAMUZI wa wanasiasa wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto kupanga mikutano tofauti kuhusu Mpango wa Maridhiano (BBI) uliashiria jinsi ukaidi wao dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta ulivyokomaa, wadadisi wanasema.

Katika mkutano waliofanya Naivasha wiki iliyopita, viongozi hao waliamua kuandaa mikutano yao ya BBI tofauti na ile ambayo tayari huendelezwa na kikundi kinachoegemea upande wa Rais kikisimamiwa na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Kulingana na wakosoaji wao, hatua hiyo ilidhihirisha wazi kwamba kikundi hicho kilicho maarufu kama Tangatanga hakiheshimu misimamo ya Rais.

Mwenyekiti wa ODM, Bw John Mbadi alisema mkutano huo wa Naivasha uliosimamiwa na Seneta wa Elgeyo Marakwet, Bw Kipchumba Murkomen ulidhalilisha mamlaka ya Rais kwani alikuwa tayari ashachagua viongozi wa kuandaa mikutano ya BBI maeneo mbalimbali ya nchi.

“Inafaa Ruto ajue waanzilishi wa BBI ni Uhuru kwa ushirikiano na Raila. Rais tayari alichagua viongozi wa kusimamia BBI katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa hivyo mtu yeyote anayetaka kuandaa mikutano, anafaa kuzungumza na waandalizi hao. Sasa kama anamteua Murkomen kusimamia mikutano eneo ambapo tayari kuna Tolgos, inaonyesha wazi anamkaidi Rais,” akasema Bw Mbadi.

Ijapokuwa wafuasi wa Dkt Ruto walidai nia yao ni kuhakikisha hamasisho ya BBI inafika maeneo mengi zaidi kwa kuongeza mikutano ya umma, wakosoaji wao wanatilia shaka sababu hizo ikizingatiwa Rais Kenyatta ndiye kiongozi wa chama cha Jubilee na aliweka mipango yake tayari.

Isitoshe, mkutano huo ulikanwa na Jubilee kupitia kwa Katibu Mkuu, Bw Raphael Tuju.

Gavana wa Elgeyo Marakwet, Bw Alex Tolgos ni miongoni mwa magavana waliotwikwa jukumu na Rais kuandaa mikutano ya BBI katika maeneo tofauti. Anasimamia eneo la Rift Valley.

Magavana wengine waliochaguliwa na Rais kwa jukumu hilo ni Charity Ngilu wa Kitui kuongoza eneo la Ukambani na Joseph ole Lenku wa Kajiado ambaye atasimamia jukumu hilo maeneo ya jamii za Wamaasai.

Katika mkutano wao, wanasiasa wa Tangatanga walikuwa wametangaza mkutano wao wa kwanza wa hadhara kuhusu BBI utafanyika Kaunti ya Nakuru mnamo Februari 8.

Kwa upande mwingine, wandani wa Rais Kenyatta na Bw Odinga walio upande wa Kieleweke wanapanga kufanya mkutano kaunti hiyo mnamo Februari 22.

Kando na kupanga mikutano tofauti na ile inayosemekana iliidhinishwa na Rais ambaye ndiye kiongozi wa chama cha Jubilee, wabunge hao walitangaza mapendekezo ambayo wakosoaji wao wanasema ni wazi yalilenga kudhalilisha mamlaka ya Rais Kenyatta katika uongozi wake wa taifa.

Mapendekezo waliyosema wanataka kupigania yajumuishwe katika ripoti ya mwisho ya BBI yanagusia changamoto zinazokumba vijana, wakulima, mahakama na matatizo kuhusu umiliki wa ardhi.

Utawala wa Jubilee umekuwa ukilaumiwa tangu ilipoingia mamlakani kwa awamu ya kwanza kuhusu ukosefu wa ajira kwa vijana, kuzorota kwa sekta ya kilimo na ukandamizaji uhuru wa mahakama.

Kwa mujibu wa viongozi wa Tangatanga, matatizo hayo yanaweza kutatuliwa kwa kutenga fedha zaidi kwenye katiba ili zifikie vijana, wakulima na idara ya mahakama.

“Yale yote waliyopitisha Naivasha ni uongo mtupu. Tunajua vyema jinsi bajeti huundwa. Bajeti haitengenezwi katika mikutano kama hiyo yao bali bungeni. Hayo mambo yao ni ya kujitafutia sifa ili waonekane wanatetea wananchi ilhali ni utapeli mtupu,” akasema Mbunge wa Kieni, Bw Kanini Kega.

Licha ya hayo, viongozi wa kikundi cha Tangatanga walisisitiza mkutano wao haukuwa na lengo lolote la kumdhalilisha Rais.

Kulingana na Mbunge wa Gatundu Kusini, Bw Moses Kuria, BBI ilileta nafasi ya watu kujadiliana kwa hivyo hilo ndilo walikuwa wakifanya Naivasha.

Huku akikana pia madai ya Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed kuwa walijadili mipango ya kumng’oa Rais mamlakani, Bw Kuria alilalamika kwamba wakati walipojitenga na masuala ya BBI, wakosoaji wao walikuwa wakiwashutumu na kisha sasa wanapokutana kujaribu kushiriki katika mpango huo, bado wangali wanalaumiwa.

“Sote tunamuunga mkono Rais. Naivasha kulikuwa na wabunge kutoka vyama tofauti, naibu rais hakuwepo. Hili suala la kumng’oa rais mamlakani ni mzaha. Kwani watu hawawezi kukaa na kujadiliana kuhusu suala jingine lolote?” akashangaa.

Naibu Rais pia alipuuzilia mbali madai ya kumdhalilisha Rais akisisitiza kwamba bado kuna ushirikiano kati yao na wataendelea kufanya kazi pamoja hadi wakamilishe hatamu yao ya uongozi.

Kufikia sasa, kikundi kinachoongozwa na Bw Odinga kimefanya mikutano kuhusu BBI katika Kaunti za Kisii, Kakamega na Mombasa.

Mkutano wa Kisii ulilenga kaunti zilizo eneo la Nyanza, ule wa Kakamega ukalenga Magharibi na wa Mombasa ulilenga Pwani.