• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 PM
Pasta Ng’ang’a aonya serikali dhidi ya kumpokonya ardhi ya kanisa

Pasta Ng’ang’a aonya serikali dhidi ya kumpokonya ardhi ya kanisa

Na ELVIS ONDIEKI

PASTA James Ng’ang’a wa Kanisa la Neno Evangelism Centre, ametangaza kuwa yuko tayari kupambana na Shirika la Kenya Railways (KR), ambalo limetangaza nia ya kutwaa ardhi ambapo amejenga kanisa lake kuu jijini Nairobi.

Mhubiri huyo jana alikashifu barua kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa KR, Bw Philip Mainga ambapo alisema kanisa hilo katika barabara ya Haile Selassie liko kwenye ardhi ya shirika hilo la serikali.

Mnamo Ijumaa, Bw Mainga alimfahamisha mwanzilishi huyo wa kanisa la Neno kwamba KR inapanga kutwaa ardhi hiyo kwa kuwa haikuwahi kubadilishwa kutoka kwa ardhi ya umma hadi ya kibinafsi.

Kwenye mahubiri yake Jumapili, Bw Ng’ang’a alisisitiza kuwa kanisa lake lilinunua ardhi hiyo kutoka kwa Benki Kuu ya Kenya.

“Mmiliki wa ardhi hii alikuwa na benki iliyodaiwa na Benki Kuu. Benki yake ilifilisika ndipo Benki Kuu ikatwaa ardhi hii, kisha ikaiuza ili kugharamia lile deni,” akasema.

Alionya kwamba kutakuwa na adhabu, ambazo hakuzitaja, dhidi ya yeyote atakayejaribu kuingilia kanisa hilo ambalo limekuwepo tangu 2003.

Kwenye barua yake, Bw Mainga alisema hatua ya kutaka Bw Ng’ang’a kurejesha ardhi hiyo ni katika juhudi za kuchukua ardhi ya reli ambayo ilinyakuliwa na watu binafsi maeneo mbalimbali ya nchi.

Alisema kwamba hakuna stakabadhi zozote kuonyesha kuwa kuna wakati ambapo KR ilikubai umiliki wa kipande hicho cha ardhi kuhamishwa kwa mtu mwingine.

Shirika hilo tayari limetwaa ardhi yake katika mji wa Kisumu ambapo mamia ya wafanyibiashara walifurushwa mwaka jana.

You can share this post!

Polisi akamatwa kwa kutia chang’aa maji

Nzige watasababishia Kenya njaa kuu, UN yaonya

adminleo