Nzige watasababishia Kenya njaa kuu, UN yaonya
VALENTINE OBARA na GITONGA MARETE
JANGA la njaa linalokodolea macho taifa kufuatia uvamizi wa nzige, sasa limevutia hisia kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw Antonio Guterres.
Huku serikali ikikiri iliweka mzaha katika kupambana na wadudu hao mapema, hatua ya Bw Guterres kuzungumzia suala hilo ni ishara ya jinsi hali ni mbaya kuliko inavyodhaniwa na wengi nchini.
Kupitia kwa mtandao wa kijamii wa Twitter, Bw Guteress alisema wataendelea kutoa usaidizi wa kuangamiza wadudu hao waharibifu kupitia kwa mashirika yake likiwemo Shirika la Chakula na Kilimo (FAO).
“Nzige ni wadudu hatari zaidi. Mkurupuko wao umesababishwa na janga kuhusu hali ya anga na unahatarisha zaidi uzalishaji wa chakula cha kutosheleza mahitaji ya wakazi wa Afrika Mashariki,” akasema.
FAO ilikuwa imetabiri mapema kwamba nzige ambao walikuwa wametoka mataifa ya Mashariki ya Kati na Somalia mwaka uliopita walikuwa wakija Kenya.
Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya, alikiri mwishoni mwa wiki kwamba kumekuwa na changamoto katika juhudi za kuangamiza wadudu hao ambao wamevamia takriban kaunti 13 sasa na wanaendelea kusafiri wakitaga mayai.
Miongoni mwa changamoto ilikuwa ni kupata kemikali zinazoweza kuua wadudu hao kikamilifu na akasema wameagiza aina mpya ya dawa kutoka Japan.
“Kulikuwa na changamoto kununua kemikali lakini tumelainisha mpango huo na tunatarajia zitawasili nchini wakati wowote kutoka sasa,” akasema mnamo Jumamosi.
Rais Uhuru Kenyatta alionekana kufedheheshwa na jinsi Wizara ya Kilimo ilivyokuwa ikipambana na nzige awali lakini amesifu mipango ambayo inaendelezwa kwa sasa.
Alipohutubu eneo la Kangeta katika Kaunti ya Meru mnamo Jumamosi, Rais alimkejeli aliyekuwa waziri wa kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri ambaye alikuwa ameambia wananchi watume picha za nzige mitandaoni watakapowaona.
Nzige hao pia wametajwa kuwa tishio la kiusalama.