Habari MsetoSiasa

Wakazi walilia Gavana Kingi awape maji

February 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES LWANGA

WAKAZI wa Malindi na Watamu, Kaunti ya Kilifi wamelalamikia uhaba wa maji unaokumba kaunti hiyo ya kitalii na kumtaka Gavana Amason Kingi asuluhishe tatizo hilo sugu.

Wakizungumza na wanahabari mjini Malindi wakiongozwa na Bw Chrispin Chenzo, wakazi hao walisema kampuni ya kusambaza maji (Mawasco) imekuwa ikipuuza kilio chao kila wakati maji yanapopotea kwa zaidi ya wiki moja licha ya wao kulipa kodi ya maji wakati ufaao.

“Hii si mara ya kwanza wala ya pili au ya tatu ambapo tumekuwa tukikosa maji bila kuelezewa sababu zitakazotuwezesha kujipanga,” alisema na kuongeza, “huenda sasa tukafanya maandamano kwa sababu mkurugenzi wa Mawasco hajaeleza wazi kwa nini hakuna maji na ni lini yatarudi.”

Juhudi za kumtafuta Mkurugenzi mkuu wa Mawasco, Bw Gerald Mwambire ofisini mwake Malindi hazikufua dafu kwa sababu hakupatikana na wala hakujibu simu.

Bw Mohamed Athman, ambaye pia ni mkazi alilaumu usimamizi wa Mawasco kwa uzembe na kumtaka Gavana Kingi aingilie kati ili kusuluhisha tatizo hilo ambalo linaathiri wakazi.

“Tunamtaka Gavana Kingi aingilie kati kwa sababu wiki moja sasa imeisha bila maji na uhaba huo umeathiri biashara kama vile hoteli, vinyozi, maduka na hata mahospitali,” alisema.

Bw Martin Kisya, ambaye pia ni mkazi alizema usimamizi wa Mawasco uliyoko unaongozya vibaya kulingana na usimamizi zilizopita.

Mnamo Juni mwaka jana, kilio cha wakazi cha uhaba wa maji kutokana na deni ya umeme ilivutia Kamati ya Kawi Bungeni ambayo ikiongozwa na naibu mwenyekiti, Dkt Robert Pukose, ambaye pia ni mbunge wa Endebess, alisinikiza ugawi wa mita za umeme katika visima vya Baricho Water Works ili kila kampuni ya maji ijilipie umeme.

Kampuni hizo za maji ambazo zinateka maji zao katika visima vya Baricho Water Works ni Mawasco, Mowasco (Mombasa), na Kimawasco (Kilifi na Mariakani).

Kampuni hizo tatu ambazo zinahudumia wakazi zaidi ya milioni moja katika kaunti ya Kilifi na Mombasa zinahudumu chini ya uongozi ya bodi ya Coast Water Service Board.