• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:30 PM
Kampeni ya kuwafaa wasichana kwa sodo yazinduliwa

Kampeni ya kuwafaa wasichana kwa sodo yazinduliwa

Mwakilishi Mwanamke wa Kaunti ya Lamu, Bi Ruweida Obbo pamoja na afisa wa watoto wa Kaunti ya Lamu, Bw Maxwell Titima na wasichana aliowaokoa katika eneo la Kiunga. Picha/ Kalume Kazungu

NA KALUME KAZUNGU

MWAKILISHI Mwanamke wa Kaunti ya Lamu, Bi Ruweida Obbo kwa ushirikiano na Wawakilishi wa kike wa Wadi za Kaunti ya Lamu wamezindua kampeni maalum inayolenga kukusanya na kusambaza sodo kwa wanafunzi wa kike na wanawake kutoka jamii zisizojiweza.

Kampeni hiyo inayotekelezwa kwenye maeneo yote ya Kaunti ya Lamu inalenga wasichana zaidi ya 1000 wa shule za msingi na upili pamoja na wanawake wengine zaidi ya1000 kutoka kwa familia maskini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Bi Ruweida alisema idadi kubwa ya wanafunzi wa kike katika kaunti ya Lamu wamekuwa wakikosa kuhudhuria masomo wakati wa hedhi kutokana na ukosefu wa sodo.

Kadhalika alisema baadhi ya wanawake katika jamii wamelazimika kutumia magodoro, vipande vya blanketi pamoja na magazeti ili kujistiri wakati msimu wao wa hedhi unapowadia.

Alisema lengo la kampeni hiyo hasa ni kuhakikisha mahudhurio ya wanafunzi wa kike shuleni yanaongezeka hata zaidi na pia kuwawezesha wanafunzi hao kubaki shuleni kuendeleza masomo yao.

Diwani wa wadi ya Hindi, Bi Anab Haji. Picha/ Kalume Kazungu

“Kama viongozi wa kike eneo hili, tumeamua kuja pamoja na kuzindua kampeni hiyo ya sodo. Tumesikitishwa na matatizo ambayo wanawake hapa Lamu hukumbana nayo kila msimu wa hedhi unapowadia.

Kuna wale ambao hutumia magodoro, blanketi au karatasi za magazeti ili kujistiri. Hilo ni jambo tunalolenga kulikomesha. Mbali na kusaidia wanafunzi zaidi ya 1000 wa kike, pia tunalenga kutoa sodo kwa wanawake zaidi ya 1000 kutoka familia maskini,” akasema Bi Ruweida.

Alisema shughuli ya kukusanya sodo tayari inaendelea kote Lamu huku kilele cha shughuli hiyo kikitarajiwa kufikia Mei 28, ambapo sodo zote zitakazokusanywa zitagawanyiwa wasichana na wanawake kutoka kila wadi kati ya wadi zote 10 za kaunti ya Lamu.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wadi ya Hindi, Bi Anab Haji, aliusifu mpango huo na kuahidi ushirikiano wa dhati ili kufaulisha shughuli hiyo.

Bi Anab aliwataka wahisani na hata viongozi wa kiume kote Lamu kujitokeza na kusaidia kufanikisha mpango huo.

Alitaja ukosefu wa sodo kuwa changamoto kubwa hasa miongoni mwa wasichana kutoka jamii za wafugaji wa kuhamahama.

“Tushirikiane kama viongozi ili kufanikisha mpango huo. Tatizo la ukosefu wa sodo lipo miongoni mwa jamii zetu na lafaa kukabiliwa na kutatuliwa kikamilifu,” akasema Bi Anab.

You can share this post!

Gor Mahia kortini kwa kukataa kuilipa hoteli

Wasomi wadai mtaala mpya wa elimu utazidisha ukabila

adminleo