• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 6:55 PM
Umaskini wazidi kutafuna Waafrika

Umaskini wazidi kutafuna Waafrika

Na PETER MBURU

UCHUMI wa bara la Afrika unazidi kukua lakini hauwafaidi mamilioni ya Waafrika maskini, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imesema.

Rais wa AfDB Akinwumi Adesina alisema licha ya ripoti kuonyesha kuwa jumla ya Utajiri wa Afrika (GDP) ulikua kwa asilimia 3.4 mwaka jana, hali hiyo haijawasaidia watu wa kawaida.

“Hakuna anayekula GDP,” Bw Adesina akasema alipokuwa akizindua mradi wa kiuchumi wa benki hiyo.

Ripoti ya Shirika la Kutafiti Uchumi wa Afrika (AEO) ya mwaka huu ilisema kuwa kwa jumla, Afrika imekua kwa kiwango cha juu, ikilinganishwa na mataifa mengine duniani.

Lakini licha ya kusema kuwa Afrika inakua, ripoti hiyo ilisema ni mataifa machache tu barani ambayo yaliripoti kupungua kwa idadi ya watu maskini, pamoja na pengo baina ya maskini na matajiri kupungua

“Maendeleo sharti yawe yanaonekana na yasawazishe wote. Sharti yawepo katika maisha ya watu,” akasema Bw Adesina.

Mataifa 18 barani yaliripoti kukua kwa uchumi, kulingana na ripoti hiyo ya AEO.

Kulingana na banki ya AfDB, uwekezaji katika sekta ya elimu, hasa kwa maskini ni mbinu moja itakayosaidia kupunguza umaskini barani Afrika, pamoja na kuziba pengo kati ya matajiri na maskini.

Inapendekeza uhamasishaji na ufadhili wa elimu katika miradi kama vile kupeana sare za bure na vitabu, pamoja na kuharamisha kazi kwa watoto na kupandisha hadhi ya ualimu.

Aidha, inazitaka serikali kuwekeza katika mitaala inayofunza mambo yanayohitajika kazini, ili wanaofuzu wasaidike katika sekta za kibinafsi.

“Afrika ina rasilimali za kutosha, na mustakabali wake uko ndani ya Waafrika…elimu ndiyo italeta usawa. Kwa kuinua wafanyakazi ndipo tutamaliza umaskini na kuziba pengo kati ya matajiri na maskini,” akasema Hanan Morsy, Mkurugenzi wa utafiti katika benki hiyo.

Mwaka jana Gavana wa Benki Kuu ya Kenya Patrick Njoroge alikuwa na maoni sawa na ya Bw Adesina aliposema kuwa wananchi hawawezi kula GDP.

Kulingana na Bw Njoroge, ukuaji wa kiuchumi unapaswa kuleta mabadiliko katika maisha ya wananchi wa kawaida kwa kupunguza umaskini na kuwawezesha kutimiza mahitaji yao ya kimsingi.

You can share this post!

Dini kuondoa hitaji la mabinti kueleza iwapo ni mabikira

Wazee wapanga kuwapatanisha Ruto na Raila

adminleo