Gor Mahia kortini kwa kukataa kuilipa hoteli
Na JOSEPH OPENDA
KLABU ya Gor Mahia huenda ikaadhibiwa na mahakama kwa kukataa kulipa deni, baada ya kupokea huduma za hoteli moja mjini Nakuru.
Mahakama ya Nakuru imewataka maafisa wanne wa klabu hiyo kufika mbele ya korti ili kueleza sababu za kutotii amri ya mahakama iliyowataka kulipa kampuni ya Donnies Bar and Hotel Sh524,730 ambazo ni sehemu ya deni baada ya kupata huduma zake.
Maafisa hao wakiongozwa na mwenyekiti Ambrose Rachier, John Pesa, Ronald Ngala na Jolawi Obongo na Kennedy Otieno, walishtakiwa kwa niaba ya klabu hiyo baada ya kususia kukamilisha deni hilo.
Hoteli ya Donnies kupitia kwa wakili wake, Bw Gordon Ogolla, iliishutumu Gor Mahia kwa kukataa kuheshimu mkataba waliokubaliana kuhusu kulipia huduma zake.
Kulingana na karatasi zilizoko kortini, hoteli ya Donnies ilikubaliana na klabu hiyo kupokea malipo kwa awamu Sh737,080 kwa huduma watakazopata mnamo Januari 15, 2015.
Aidha korti iliambiwa kwamba klabu hiyo ililipa Sh300,000 pekee kisha ikakataa kukamilisha deni lililokuwa limebaki.
Mnamo Juni 2017, korti iliamuru maafisa hao kukamilisha deni hilo.
Wenye hoteli hiyo walirudi kortini kutaka klabu hiyo iadhibiwe kwa kukosa kutii amri ya mahakama.
“Unahitajika kufika mbele ya korti hii mnamo Aprili 17 kueleza korti sababu zinazoweza kufanya msiadhibiwe,” ilisoma sehemu ya amri hiyo.