#IfikieWazazi: Kizazi hiki cha dijitali kitaponzwa na ngono
Na GEOFFREY ANENE
WAKENYA wameamua kuwaanika matineja wanaochapisha picha wakiwa nusu uchi na zingine za ngono katika mitandao ya kijamii kwenye umma ili kuwaaibisha baada ya kuona vitendo vyao vimepita mipaka.
Kwa kipindi kirefu Alhamisi, watumiaji wa mitandao ya kijamii walichapisha picha pamoja na video za makinda hao wakisherehekea uchi wao, wakitumai wazazi na walezi wao wataweza kuwatambua na kuwakanya dhidi ya tabia hiyo.
Tovuti ya Taifa Leo ilifanikiwa kung’amua kiasi cha uchi kilichokuwa kikizungumziwa katika majibizano kwenye mtandao wa Twitter.
Picha zilizochapishwa zilikuwa za kutisha kwa wazazi na walezi, huku vijana hao wakionekana kuvalia njuga ngono katika umri mdogo. Nyingi ya picha hizo zinahusu usisimuaji wa hisia za mahaba, densi za uchi na ngono.
Mambo yalianza pale msichana mmoja alichapisha video akiwakejeli wakosoaji wanaochemkia wanawake walio na umri mdogo kuchapisha picha zao za uchi kwenye mitandao.
Msichana huyo, ambaye hakutambuliwa, anatusi “wanaomchukia” na kuwataka wajishughulishe na mambo mengine akisema ni uamuzi wake kuonyesha watu mwili wake.
“…Nikiamua kuonyeshana mwili wangu, ni wangu. Nitaonyeshana hadi siku nitaaga dunia…,” aliapa.
Video ya msichana huyo ilisambaa kwa haraka kupitia hashtegi ya #ifikiewazazi ambayo watumiaji wa mitandao ya kijamii walianza kueneza picha za wavulana na wasichana wanaochapisha picha zao, baadhi yao wakiwa nusu uchi.
Wakenya wengi kwenye kundi la Kenyans on Twitter (KOT) walikashifu wavulana na wasichana hao, huku wengine wakisalia vinywa wazi kutokana na kiasi cha uozo wa tabia unaoonyeshwa na kizazi hichgo kinachojigamba kuwa: “Sisi ni dijitali, analogi hamtuwezi.”
Picha nyingi na video zilizosambazwa kwenye Twitter kupitia hashtegi #ifikiewazazi ni za kutisha sana, kiasi kwamba haziwezi kuchapishwa kwenye tovuti hii.