• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Ajeruhiwa baada ya boti kushika moto baharini

Ajeruhiwa baada ya boti kushika moto baharini

Na KALUME KAZUNGU

MWANAMUME amejeruhiwa boti alimokuwa amekaa iliposhika moto ghafla na kulipuka mjini Lamu.

Bw Shafi Mawiyawiya amenusurika baada ya injini ya boti yake inayotumia mafuta ya petroli kushika moto ghafla na kuchomeka.

Hata hivyo, wakati wa tukio hilo, Bw Mawiyawiya amechomeka vibaya kwenye mguu na mkono wake wa kushoto kabla ya kuokolewa.

Boti ilikuwa imeegeshwa ndani ya Bahari Hindi, karibu na ufuo ulioko mkabala na mji wa kale wa Lamu.

Ilichukua takriban saa moja kwa wapigambizi waliojitolea kutumia maji ya Bahari Hindi kuuzima moto huo ambao karibu uenee kwenye boti na mashua zingine zilizokuwa karibu.

Aliyejeruhiwa katika mkasa huo alikimbizwa kwenye hospitali kuu ya rufaa ya King Fahad mjini Lamu.

“Ilikuwa yapata saa kumi na nusu hivi ambapo tulishtukia moto mkubwa ukitoka kwa boti iliyokuwa imeegeshwa baharini. Tuliona mwanamume akitapatapa jinsi ambavyo angejinasua kutoka ndani ya boti hiyo,” amesema mmoja wa manahodha wa boti mjini Lamu, Athman Musa.

Akaongeza: “Ghafla tuliingia majini na kuelekea kwenye boti hiyo na kumuokoa jamaa huyo ambaye tulimwagiza kujirusha baharini na kisha nasi tukauzima moto huo mkubwa kwa kutumia maji ya bahari. Mwathiriwa alichomeka mguu na mkono lakini tukampeleka hospitalini anakopokea matibabu.”

Kufuatia tukio hilo, Mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki wa Boti na Mashua, Kaunti ya Lamu, Hassan Awadh, amewatahadharisha mabaharia na wasafiri wengine dhidi ya kuvuta sigara wakati wakisafiri kwa kutumia boti na mashua ambazo nyingi hutumia injini za petroli.

Kulingana na Bw Awadh, kuvuta sigara ndani ya boti au mashua huenda kukasababisha ajali ya moto na hata maisha kupotezwa baharini.

“Lazima tujiepushe na mambo yanayohatarisha maisha yetu na abiria. Haistahili kuvuta sigara unaposafiri kwenye chombo kinachotumia petrol. Utasababisha moto, ajali na maafa. Tuepuke kabisa mambo yanayohatarisha maisha yetu ili usafiri wetu uwe shwari na salama,” akasema Bw Awadh.

Takribani asilimia 99 ya usafiri, Kaunti ya Lamu hutegemea sana bahari, ambapo vyombo, ikiwemo boti, mashua na jahazi hutumika.

You can share this post!

RIZIKI: Mwalimu aliyejinyima mengi kujiendeleza kielimu...

GORP FC yalenga kusajili matokeo mazuri

adminleo